25 July 2013

MBOWE AWATUNISHIA MSULI POLISINa Stella Aron
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ameendelea kuliwekea ngumu Jeshi la Polisi nchini kwa kukataa kukabidhi mkanda wa video unaoonesha tukio la mlipuko wa bomu uliotokea kwenye mkutano wa CHADEMA, mkoani Arusha wakati wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi wa kata nne za madiwani.
Mbowe aliripoti Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam jana kufuatia barua aliyoandikiwa na jeshi hilo likimtaka afike na kuwasilisha mkanda huo, anaodai anao. Akizungumza na gazeti hili Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa CHADEMA, John Mnyika, alisema barua hiyo ya Polisi ilikuwa ikieleza kuwa endapo atashindwa kuwasilisha mkanda huo atakuwa ametenda kosa la jinai.

Mnyika alisema Mbowe alienda mwenyewe Polisi akiwa na wakili wa CHADEMA, Peter Kibatala na viongozi wengine wa chama. Mnyika alisema Mbowe aliwaambia Polisi kuwa ushahidi wa mkanda huo hataukabidhi kwao, kwani wao ni miongoni mwa watuhumiwa. "Amewaambia kama ni kosa la jinai libaki hivyo, lakini hawezi kuwakabidhi mkanda huo kwa kuwa na wao ni miongoni mwa watuhumiwa," alisema Mnyika.
Kwa mujibu wa Mnyika, Mbowe ameendelea na msimamo wake kuwa mkanda huo ataukabidhi kwa Tume ya Kijaji itakayoundwa na si vinginevyo. Aliongeza kuwa baada ya maazimio ya Kamati Kuu ya CHADEMA iliyokutana hivi karibuni, Mbowe alimwandikia Rais Jakaya Kikwete, barua ya kumtaka aunde Tume ya Kijaji ya kuchunguza tukio hilo, lakini hadi sasa bado haijajibiwa.
Katika tukio hilo la mlipuko wa bomu watu wanne walifariki na wengine wengi kujeruhiwa. Tangu wakati huo, Mbowe amekuwa akidai kuwa ana ushahidi wa video wa tukio hilo, lakini amekataa kuukabidhi kwa polisi kwa kile anachodai kwamba na wao ni miongoni mwa watuhumiwa. "Kwa hiyo amewaambia Polisi kuwa bado jambo hilo ameandikiwa Rais Kikwete na bado hajajibu hivyo hawezi kufanya hivyo," alisema Mnyika akimnukuu Mbowe.
Alisema baada ya mazungumzo ya kina kati yake na Polisi, walikubaliana kwamba Mbowe aeleze msimamo wake huo kwa maandishi na kuwapelekea Polisi kesho na baada ya hapo watajua la kufanya.
Alisema baada ya mazungumzo hayo Mbowe aliondoka na yupo huru

No comments:

Post a Comment