Na Rehema Mohamed
SHAHIDI wa 10 katika kesi ya wizi wa
tani 26 za madini aina ya shaba inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Pwani, (COREFA), Hassan Othman 'Hassanoo' na wenzake wawili,
Rahim Jeta (38) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shaba hiyo ya
wizi ilihifadhiwa katika yadi ya mshtakiwa wa pili, Dkt. Najim Msenga baada ya
Hassanoo kumuomba.
Shahidi huyo ambaye alikuwa Mkurugenzi
wa Kampuni ya Usafirishaji wa Mizingi ya Libert Express iliyohusika kusafirisha
shaba
hiyo, alieleza hayo mahakamani hapo jana wakati akitoa ushahidi wake
mbele ya hakimu Devotha Kisoka.Huku akiongozwa na Wakili wa Serikali
Tumaini Kweka, Jeta alidai kuwa baada ya kupata taarifa za gari lao, T 821 DCL
Scania lililobeba shaba
hiyo kutofika bandarini walilifuatilia kupitia njia ya mtandao na kubaini
lilipitia barabara ya Bagamoyo hadi eneo la Bahari Beach katika Yadi ya Najim.
Alisema walipofika katika yadi hiyo,
wakiwa na polisi kutoka kituo cha Oysterbay kabla ya kufanya ukaguzi, ndipo
mmoja wa mapolisi hao walipompigia simu Msenga, kumtaka afike hapo lakini
hakufika kwa sababu alikuwa Tanga katika msiba.Shahidi huyo alisema kwa mujibu wa
polisi hao, mshtakiwa wa tatu (Msenga) alikana kuhusika na shaba hiyo, ila
anachokifahamu ni kwamba Hassanoo alimuomba ahifadhi mzigo huo katika yadi
yake.
Alidai kuwa shaba
hiyo ilikuwa ikisafirishwa kutoka Solowezi,
Zambia kuja
jijini Dar es Salaam na ilitakiwa kushushwa katika bandari kavu ya Tanzania
Road Haulage (TRH).Naye shahidi wa tisa ambaye ni Ofisa
Utumishi wa Kampuni ya Libert - Express, Solomon Makogo (47) alidai kuwa
walipofika katika yadi ya Najim, walikuta shaba hiyo imefunikwa kwa turubai
jekundu na kwamba aliipiga picha.
Mbali na Hassanoo, washtakiwa wengine
katika kesi hiyo ni mfanyabiashara Wambura Kisiroti (32) na Dkt. Msenga (50).Inadaiwa kuwa Agosti 26, 2011 Bahari
Beach washtakiwa hao waliiba tani 26 za madini ya shaba
yenye thamani ya sh. milioni 400, mali
ya Kampuni ya Liberty Express Tanzania Ltd yaliyokuwa yakisafirishwa kutoka Zambia kwa lori
kuja Dar es Salaam.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 6, mwaka huu
itakapoendelea kusikilizwa
No comments:
Post a Comment