31 July 2013

SERIKALI TATU NI KICHEKESHO - BARONGO



Na Rehema Mohamed

ALIYEKUWA Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma Kapteni mstaafu, John Barongo amesema mapendekezo ya kubadilisha Muungano uwe wa Serikali tatu ni kichekesho hasa kwa kipindi hiki ambapo Afrika inafikiria kuwa na serikali moja.


Kapteni Barongo aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu rasimu ya Katiba Mpya na maoni mbalimbali yanayotolewa kuhusu muundo wa Katiba Mpya.Kapteni Balongo alisema, wazo la kuwepo kwa serikali tatu ni la baadhi ya viongozi wachache wanaotaka madaraka huku wengine wakizungumzia kuundwa kwa Katiba ya Tanganyika ili wapate uongozi badala ya kuzungumzia matatizo ya wananchi.

Pamoja na hilo, Kapteni Balongo alikiri kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una matatizo na kusema kuwa hizo ni changamoto ambazo zinahitaji ufumbuzi wa pamoja na si kuwa na serikali tatu.Alisema, huko nyuma kuna baadhi ya nchi zilijaribu kuwa na muundo wa serikali tatu na kushindwa kuziendeleza huku akitolea mfano wa nchi ya Egypt na Syria ambazo ziliwahi kuunda Shirikisho la Syria (United Arab Republic) ambapo mwezi Septemba mwaka 1961 Mkuu wa Majeshi wa Syria alijiondoa katika shirikisho hilo na ukawa mwisho wa muungano huo.

"Nchi nyingine ni Mali na Senegal ambapo wao waliunda Mali Federation wakati huo Mali ikiitwa French Sudan, akachaguliwa Modibo Keita akawa Rais wa serikali hizo tatu na matokeo yake Rais wa Senegal wakati huo Leopold Sedar Senghor alijiondoa na ukawa mwisho wa shiririkisho hilo,"alisema Kapteni Barongo

Alisema kuwa, Watanzania wanatakiwa wajifunze kutoka katika nchi hizo kwani kuwepo na serikali hizo ni mzigo kwa wananchi kuhudumia marais wa serikali tatu hasa kwa wakati huu ambapo uchumi wa nchi si mzuri.Alisema kuwa, ni bora nchi ikabaki na serikali mbili kama ilivyo sasa na kisha kutatua mambo yanayokwamisha Muungano kuliko kuruhusu tatu ambazo zinaweza kuongezeka na kuwa nne kutokana na mapendekezo ya watu.

Hata hivyo, alitaka suala la ardhi lisiwe sehemu ya Muungano kwa sababu Wazanzibar wengi wanakuja Tanganyika na kujenga ambapo kwa Watanganyika inakuwa vigumu kupata ardhi Zanzibar.Akizungumzia mchakato wa Katiba mpya alisema, hakuna ulazima wa nchi ikawa na Katiba Mpya ifikapo mwaka 2015 na badala yake yaangaliwe mapungufu yaliyopo katika katiba ya sasa na kufanyiwa marekebisho.

"Mapungufu katika katiba ya sasa yapo ila kinachotakiwa ni kubainisha mapungufu hayo na kuyafanyia kazi na si kuiga nchi za jirani kama Kenya walivyobadili katiba yao, nadhani tungekuwa na katiba nzuri zaidi miaka 10 kutoka sasa,"alisema.

Katika hatua nyingine, Kapteni Barongo amekitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kusimamia, amani, mshikamano na kupambana na ufisadi wa kila aina,kuwahudumia wananchi katika kupata haki zao na kuwakataa viongozi wanaotumia vitu hivyo kwa masilahi yao.

Alisema kuwa, wananchi wanajua nani anayefaa kuongoza nchi na kwamba Rais wa nchi hii anaweza kutoka chama chochote isipokuwa rais bora anatokea CCM.

Alisema kuwa, viongozi wa CCM lazima wabadilike na kuachana na kuongoza kwa mazoea ikiwa ni pamoja na kufahamu aina ya rais anayetakiwa kusimama mwaka 2015 asiyekuwa wa kununua watu bali wananchi wampende wenyewe

No comments:

Post a Comment