31 July 2013

NTAGAZWA ANA KESI YA KUJIBU



 Na Rachel Balama
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira wa zamani, Arcado Ntagazwa (65) na wenzake wawili wanaokabiliwa na shtaka la kujipatia mali ya zaidi ya sh.milioni 74 kwa njia ya udanganyifu wamepatikana na kesi ya kujibu.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu Gene Dudu alisema kuwa, kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka mahakamani hapo unaonyesha kwamba washtakiwa wana kesi ya kujibu.
"Mahakama imeona washtakiwa wote wana kesi ya kujibu kutokana na ushahidi wa upande wa Jamhuri hivyo kila mtu atajibu shtaka mahakamani", alisema Hakimu huyo.
Katika kesi hiyo, upande wa serikali unaongozwa na Wakili Charles Anindo ambapo ulikuwa na mashahidi watano.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Dkt. Webhale Ntagazwa (29) na Seneta Miselya (60).
Washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kujipatia mali ya zaidi ya sh.milioni 74 kwa njia ya udanganyifu.
Aidha, walidaiwa kuwa Oktoba 22, 2009 maeneo ya Mikoroshini Msasani katika Wilaya ya Kinondoni, washtakiwa kwa nia ya udanganyifu walijipatia kofia 5,000 na fulana 5,000 kutoka kwa Noel Severe zenye thamani ya sh. milioni 74.
Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walimdanganya Severe kuwa bidhaa hizo wangezilipa baada ya mwezi mmoja tangu kupewa mzigo huo, jambo ambalo hawakulitekeleza.
Hata hivyo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 2, mwaka huu ambapo washitakiwa wataanza kujitetea.

No comments:

Post a Comment