CAIRO, Misri
RAIS wa
Misri, Mohammed Morsi, amesisitiza kuwa yeye ndiye kiongozi halali wa Taifa
hilo ambapo maandamano kati ya wapinzani na wafuasi wake, yameendelea
kusababisha vifo zaidi nchini humo.
Alisema jeshi la nchi hiyo haliwezi kutatua mgogoro wa kisiasa
nchini humo na hawezi kuamrishwa na yeyote ambapo mpango wa jeshi hilo kuingilia
kati, itazua hali ya sintofahamu.
Rais Morsi aliyasema hayo juzi usiku katika hotuba yake na
kuwataka waandamanaji kuwa watulivu. Hadi jana watu 16 wameripotiwa kufa katika
maandamano ya wafuasi wake.
Awali, jeshi la nchi hiyo lilitoa saa 48 kwa Rais Morsi awe
ametatua mgogoro wa kisiasa uliopo nchini humo lakini kiongozi huyo amepinga
onyo la jeshi dhidi ya utawala wake.
Wakati Rais
Mosri akiendelea kukabiliwa na shinikizo hilo, maofisa zaidi wa Serikali yake
wameendelea kujiuzulu nafasi zao likiwemo Baraza la Mawaziri.
Chama cha
upinzani cha National Salvation Front, kilisema kinaunga mkono tamko la jeshi,
lakini hakipo tayari kuona jeshi hilo likifanya mapinduzi ya kijeshi.
Jumapili
iliyopita, mamilioni ya wananchi nchini humo walifanya maandamano wakimtaka
Rais Morsi ajiuzulu ambapo maandamano mengine makubwa yalifanyika Jumatatu wiki
hii.
Taarifa
zaidi zinadai kuwa, watu wanane waliuawa baada ya waandamanaji kuvamia Makao
Makuu ya Chama cha Muslim Brotherhood. Wapinzani wa Rais Morsi, wanamkosoa kwa
kuweka masilahi ya chama mbele na kuwapuuza watu wasiokiunga mkono chama hicho.
Rais Morsi alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa
Kiislamu katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Juni 30,2012 baada ya kuibuka
mshindi. Uchaguzi huo ulifanyika baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Hosni
Mubarak kuondolewa madarakani
No comments:
Post a Comment