30 July 2013

MWANASHERIA MKUU AWAPA ONYO POLISI



 Na Elizabeth Joseph, Dodoma
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Frederick Werema, amewaonya na kuwataka wapelelezi nchini kuacha tabia ya kubambikiwa kesi watu wakati hawana hatia yoyote.Jaji Werema, alitoa onyo hilo wakati akifungua mkutano wa kwanza wa Mawakili wa Serikali Wafawidhi na Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa uliofanyika jana, mjini Dodoma.

Alisema kumekuwa na tabia ya uonevu wa kuwabambikia kesi watu, vitendo ambavyo amevipinga vikali kuwataka kutumia weledi wakati wa kumkamata wahalifu.“Tusitumie nguvu kumkamata mhalifu wala kulipa kisasi kwa kuwabambikiwa kesi pamoja na kumkamata mtu kama hamna ushahidi wa kutosha, kwani kufanya hivyo kutaleta uhusiano mzuri na wananchi,” alisema Jaji Werema.
Aliwataka wanasheria na wakuu wa upelelezi hao kuhakikisha upelelezi na ushahidi wanaoutaka unapatikana haraka pamoja na kuwafahamisha washtakiwa hatua waliyoifikia na haki zao kisheria, ili kuleta imani kwa watu wanaowatumikia pamoja na kuondoa manung’uniko miongoni mwao.
Jaji Werema pia aliwataka wakuu hao kufuata maadili ya kazi zao, ikiwa ni pamoja na kutunza kumbukumbu na majalada ya kesi mbalimbali, kwani ni wajibu wao kuyalinda kwa kuyahifadhi katika hali nzuri.
Mbali na hilo, alikemea vitendo vya baadhi wa mawakili wafawidhi na wakuu wa upelelezi kuacha tabia ya kuuza kesi kwa watu kwa kupokea rushwa jambo ambalo linavunja miongozo ya kazi wanayosimamia

No comments:

Post a Comment