ALIYEKUWA Rais wa Misri,Dkt.Mohammed Morsi, alizaliwa Agosti,1951 katika
jimbo la Shargiya lililopo katika eneo la Mto Nile, Kaskazini mwa nchi hiyo.
Jina kamili la kiongozi huyo ni Moham med
Mohammed Morsi Issa Ayyat ambaye ni rais wa kwanza kuweka historia nchini humo
kuchaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Juni, 2012 kwa kufuata demokrasia baada
ya kuondolewa madarakani Rais Hosni Mubaraka ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa
zaidi ya miaka 30.
Morsi pia aliweza kuweka historia kuwa
rais wa kwanza kuongoza kwa kufuata sheria za Kiislamu chini ya chama chake cha
Udugu wa Kiislamu (Muslim Brotherhood).
Kwa upande wa elimu yake, mwaka 1982
Dkt.Morsi alifanikiwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika fani ya
Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Southern California kilichopo katika Jimbo la
Carifonia nchini Marekani.
Kabla ya hapo mwaka 1978 Dkt. Morsi
aliwahi kutunukiwa shahada ya Uzamili katika fani ya Uhandisi katika Chuo Kikuu
cha Cairo nchini Misri kabla ya kwenda Marekani.
Awali mwaka 1975 kiongozi huyo, aliyedumu
madarakani kwa mwaka mmoja, alitunukiwa shahada ya Uhandisi katika chuo hicho
hicho cha mjini Cairo mji Mkuu wa Misri.
Baada ya mwaka mmoja tangu kupata PhD,
Dkt. Morsi alianza kufanya kazi kama Profesa Msaidizi katika Chuo Kikuu cha North
Ridge nchini Califonia, ambako alitumikia cheo hicho hadi 1985.
Baada ya kuacha kazi, Dkt. Morsi alirudi
nchini kwake Misri na kufanya kazi katika Chuo Kikuu cha Zagazig kama mkuu wa
kitengo cha Wahandisi kati ya 1985 hadi 2010.
Wakati yupo jimboni Carifonia, Dkt. Morsi
aliweza kupata watoto wawili kati ya watano aliokuwanao ambao wana uraia wa
nchi hiyo.
Mwaka 1977, Dkt. Morsi alijiunga na
harakati za kisiasa kama mwanachama wa chama kinachosimamia sera za Kiislamu
cha Udugu wa Kiislamu.
Mbali na hilo, Dkt. Morsi alichaguliwa
kama mwanachama wa Mkutano wa Kimataifa wa Vyama vya Siasa na Taasisi na
mwanachama mwanzilishi wa kamati ya mradi wa Misri wa kupinga uongozi usiofuata
demokrasia (Zionism).
Mwaka 2000 mpaka 2005, Dkt. Morsi
alifanikiwa kuwa mbunge binafsi katika bunge la nchi hiyo tangu chama chake
kizuiliwe kuteua wagombea urais, kwa mujibu wa sera zilizowekwa na Rais wa
zamani, Hosni Mubarak.
Wakati wa uongozi wa Hosni Mubarak,Dkt.
Morsi alikamatwa na jeshi la nchi hiyo kutokana na kupinga serikali iliyokuwa
madarakani.
Juni 24, 2012, Morsi aliweza kuweka
historia nchini Misri baada ya kuwa rais wa kwanza wa kuchaguliwa kwa kufuata
demokrasia.
Pia aliweza kuweka historia kuwa rais wa
kwanza kuongoza kwa kufuata sheria za Kiislamu nchini chini ya chama cha Muslim
Brotherhood.
Bw.Morsi ni rais wa tano kuongoza nchi
hiyo ila ni wa kwanza asiyewekwa na jeshi hivyo uchaguzi wake ulitengeneza sura
mpya ya nchi hiyo katika historia.
Baada ya ushindi huo, katika hotuba yake
alisikika akisema kuwa yeye ni rais wa wa-Misri wote na atashirikiana nao
katika kulisukuma gurudumu la nchi hiyo ili iweze kusonga mbele kiuchumi
tofauti na uchumi walionao pamoja na kudumisha umoja wao.
Bw.Morsi alianza kazi kwa kasi zaidi,
kwani Agosti, 2012 aliwatimua baadhi ya maofisa wa jeshi kama rais wa nchi
hiyo.
Moja ya ahadi zake Bw.Morsi ni kuinua
uchumi wa nchi hiyo ahadi ambayo imeonekana kushindwa kuitekeleza kwa wananchi
wake na kusababisha Wamisri kuanza maandamano ya kutaka aondoke baada ya kukaa
mwaka mmoja madarakani.
Hivyo kutokana na hali hiyo Bw.Morsi
alionekana kukaidi maamuzi ya wananchi na kuhoji kuwa yeye ndiye rais halali wa
nchi hiyo.
Kutokana na pingamizi lake likasababisha
maandamano yaliyodumu kwa siku nne kumshinikiza atoke madarakani katika viwanja
vya Tahrir Square katika mji mkuu wa nchi hiyo
Hivyo ili kunusuru madhara ambayo
yangeweza kutokea Mkuu wa Jeshi la nchi hiyo Bw.Abdel- Fatah El-Sis walimpa
masaa 48 kujiuzuru ili kuleta amani katika nchi hiyo amri ambayo alipinga na
kusababisha kupinduliwa rasmi hapo juzi.
Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Jeshi hilo
amesikika akitangaza uamuzi wa jeshi kuchukua madaraka ili kuendelea kulinda
amani kwa wananchi wa nchi hiyo.
Waandamanaji hao inasadikiwa kuwa
wamesikika wakidai kuwa kiongozi huyo alikuwa anawawezesha watu wa chama chake
na kuwasahau wananchi wengine kama rais.
Hadi leo jeshi la nchi hiyo limemteua Jaji
Mkuu wa Mahakama ya Katiba Misri, Adly Mansour kuongoza kwa muda hadi pale
utaratibu utakapokamilika ambaye kabla ya uteuzi huo aliteuliwa kuwa jaji wa
mahakama hiyo Juni 30, mwaka huu kabla ya uteuzi huo.
Moja ya taratibu hizo ni pamoja na
uandaaji wa katiba kutokana na nchi hiyo kutokuwa na katiba inayosimamia
mamlaka ya nchi hiyo.
*Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa
vyombo vya habari
No comments:
Post a Comment