Na Heckton Chuwa,
Moshi
MGOMO mkubwa wa usafirishaji unaoyahusu
magari makubwa aina ya Coaster umetokea mjini Moshi Mkoa wa Kilimanjaro na
kusababisha adha kubwa kwa wananchi waliokuwa wakisafiri katika Wilaya za Moshi
Mjini na Wilaya ya Rombo, mkoani humo.Mbali na adha
hiyo kwa abiria, vurugu kubwa zilitokea kati ya viongozi na madereva wa magari
makubwa yanayofanya safari kati ya Rombo na Moshi mjini na wale wa magari
madogo aina ya Noah.
Wakati mgogoro
huo ukiendelea mmoja wa watu anayedaiwa kuwa ni dereva wa gari aina ya Noah
alikimbilia kwenye hoteli ya jirani na kutoka na kisu na kumfuata kiongozi wa
Chama cha Wenye Magari Makubwa Aina ya Coaster, Linus Kilawe kwa lengo la
kumdhuru kabla ya kuzuiwa na wenzake.
Akizungumzia mgomo huo, Kilawe alisema
wamiliki wa magari hayo wameamua kuuitisha kufuatia malalamiko yao kuhusiana na
wenzao wanaomiliki na kuendesha biashara ya usafiri wa Noah kutokuzingatiwa na
mamlaka husika.
"Hawa wenye Noah wanaenda umbali
ambao hawaruhusiwi kisheria, hawana sare, wanatoza nauli bila ya kutoa tiketi
kwa abiria huku wakibeba abiria wengi kuliko wale wanaoruhusiwa kisheria kwenye
magari hayo. Wenye magari makubwa wakifanya makosa hayo huwa wanachukuliwa
hatua za kisheria," alisema.
Kilawe aliendelea kusema kuwa, kwa wenye
magari ya Noah kuruhusiwa kwenda umbali zaidi ya kilomita wanazoruhusiwa
kisheria kumesababisha wenye magari makubwa kukosa abiria na kujikuta
wakikusanya abiria njiani kama vile daladala wakati safari zao ni za umbali
mrefu.
Alisema, hatua ya magari aina ya Noah
kuruhusiwa kufanya biashara hiyo bila kulipia gharama za kisheria kama zile
wanazotozwa wenye magari makubwa kunainyima serikali mapato ya kihalali huku
mamlaka zenye kuhusika likiyafumbia macho mambo hayo.
Alisema, tayari wameshakutana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt.
Ibrahim Msengi ambapo walipeleka mapendekezo yao yanayotaka pamoja na mambo
mengine, wenye magari makubwa na wale wa Noah wakubaliwe kupakia abiria kwa
zamu wakati masuala mengine yakifanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment