IMEELEZWA kuwa Tanzania inakabiliwa na upungufu wa tani 220,000 za sukari
kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa sukari ikiwa ni
pamoja na wakulima kutowezeshwa katika masuala ya uzalishaji.
Hayo yamebainishwa jana na mchambuzi na
mshauri wa masuala ya chakula na kilimo Afrika kutoka Benki ya Kimataifa ya
Robo, Sierk Plaat wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya
37 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba, kufuatia utafiti uliofanywa na benki ya
NMB kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Alisema sukari inayozalishwa nchini ni
tani 300,000 wakati mahitaji ni tani 520,000 ili iweze kukidhi mahitaji ya
wananchi.
“Pengo hili la uzalishaji endapo wakulima
watasaidia kuondokana na changamoto zinazowakabili itasaidia kuachana na
biashara za kuagiza sukari nje ya nchi,”alisema Plaat.
Alisema ana imani sukari inayozalishwa
nchini ni bora lakini kutokana na sababu mbalimbali zimechangia upungufu wa
uzalishaji hali ambayo inachangia kutegemea zaidi sukari inayoagizwa kutoka
nje.
Kwa upande wake, Calo Nyangaro ambaye
alifanya utafiti wa stakabadhi ghalani alisema, katika utafiti wao wamebaini
utaratibu wa stakabadhi ghalani unawasaidia sana wakulima endapo utasimamiwa
vizuri na kuzingatiwa.
Alisema katika utafiti walioufanya kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali walitaka kubaini kama utaratibu wa stakabadhi
ghalani unatoa tija kwa wakulima kwa upande wa wakulima wa korosho, ufuta,
mpunga na mazao mengineyo.
Isack alisema katika utafiti huo
walioufanya maeneo mbalimbali nchini wamebaini unatekelezeka kwa kiwango cha
juu mbali ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo wakulima.
Naye, Meneja Mkuu Kitengo cha Kilimo NMB,
Robert Pascal alisema benki ya NMB iliamua kufanya tafiti mbalimbali kwa lengo
la kuisaidia jamii ya wakulima nchini na kunyanyua pato la taifa.
Alisema hadi sasa wametoa mkopo wa sh. bilioni 116 kwa
wakulima na kuzifikia kaya 500 nchi nzima.
No comments:
Post a Comment