24 July 2013

KIKWETE AJITOSA SAKATA KODI ZA SIMU NCHININa Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete, ameagiza Wizara za Serikali zinazohusika na kodi na mawasiliano pamoja na kampuni za simu za mikononi nchini kukutana mara moja kutafuta jinsi gani ya kumaliza mvutano wa kodi mpya ya kadi za simu hizo za mikononi.

Rais Kikwete alitoa maelekezo hayo jana jioni wakati alipokutana na viongozi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na wawakilishi wa kampuni za simu Ikulu, Dar es Salaam.
Rais Kikwete alisema lengo kuu la mkutano huo wa pamoja kati ya Wizara hizo za Serikali na kampuni za simu ni kupendekeza jinsi gani ya kuziba pengo la sh. bilioni 178 ambazo zitapotea katika Bajeti iwapo kodi hiyo kwa kadi za kuongelea za simu za mikononi italazimika kufutwa na Serikali kupitia marekebisho kwenye Mswada wa Fedha wa Bajeti ya Mwaka 2013/2014.
Rais Kikwete aliwaambia wawakilishi wa pande hizo mbili kuwa huwezi tena kuifuta moja kwa moja kodi hiyo bila kutafuta njia nyingine za kupata fedha za kujaza pengo hilo la sh. bilioni 178 ambazo tayari Bunge limezipangia matumizi.
"Nawaombeni kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili yenu pamoja tutafute namna gani tunaweza kujaza pengo hili la sh. bilioni 178 endapo tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha wananchi mzigo mzito na kuwa pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu," alisema Rais Kikwete.
Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014, Serikali imeweka kodi ya Sh. 1,000 kwa mwezi kwa kila mtumiaji simu kwa ajili ya kufanya mawasiliano kwa kutumia simu ya mkononi.

No comments:

Post a Comment