24 July 2013

SERIKALI YABAINI VYANZO VIPYA UZALISHAJI UMEME



 Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imeanza mchakato wa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbadala nchini, ukiwemo wa kutumia joto la ardhini ili kukabiliana na tatizo la nishati hiyo nchini.
Katika utekelezaji huo tayari Serikali imeanza utafiti pamoja na mazungumzo na wataalamu kutoka nchi mbalimbali na wawekezaji kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kutumia chanzo kipya cha umeme joto nchini.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, wakati akizungumza na gazeti hili. Alisema kwa kutumia maeneo yaliyoko katika bonde la ufa nchini, kuna uwezekano mkubwa wa kuzalisha umeme ambao utachangia kupunguza matatizo ya umeme nchini.
"Kwa muda mrefu tumekuwa tukitegemea vyanzo vikubwa kupata umeme, ni wakati mwafaka sasa Watanzania tubadilike," alisema Prof. Muhongo na kuongeza;
"Kuna vyanzo mbalimbali vya umeme na kwa muda mrefu tumekuwa tunategemea maji zaidi." Waziri Prof. Muhongo aliongeza kuwa Serikali imeamua kutangaza vyanzo vingine vya umeme na kuvitaja kuwa ni gesi asilia, makaa ya mawe, nishati jadidifu na maji.
Al i s ema v y a n z o v y o t e vilivyotajwa vimeweza kutumika kwa kiasi kikubwa isipokuwa nishati jadidifu.
"Nishati jadidifu ni pamoja na upepo ambao tumeanza kutumia mkoani Singida,jua, joto ardhi na mwingine," alisema Prof. Muhongo na kusisitiza kuwa serikali imeamua kufanyia kazi chanzo hicho kipya cha joto asilia (geothermal energy) na kwamba wataalamu wetu watatakiwa kuelimishwa kuhusiana na nishati hiyo.
Waziri Muhongo alitoa mifano ya nchi jirani ya Kenya ambao wanazalisha si chini ya megawati 600, Ethiopia nao wanazalisha umeme kwa kutumia joto ardhi.
Alisema Serikali katika mpango wake wa miaka 10 na 20 imeamua kuweka nguvu katika eneo hilo ambapo baadhi ya wataalamu kutoka nchi mbalimbali wameamua kushirikiana na wizara katika kutafiti na kuzalisha umeme.
"Juzi nimeongea na Waziri wa Mambo ya Nje wa New Zealand ambaye alionesha nia ya kuleta wataalamu nchini‚" alisema Waziri Prof. Muhongo na kuongeza kuwa kampuni ya Marekani ya ORMT imekubali kuzalisha umeme wa joto asilia nchini na kwamba hiyo itaendana na mpango wa Rais Barack Obama wa Marekani wa Power Africa.
Wengine ni pamoja wataalamu kutoka Ujerumani na kampuni ya TOSHIBA ya Japan iliyokuwepo nchini na kwamba wamekubali kusaidia kutafiti vyanzo vingine na kujenga mitambo.
Maeneo yenye uwezo wa kuzalisha umeme ni pamoja na mikoa ya Mbeya, Arusha, Manyara, Mkoa wa Pwani na maeneo yote yaliyoko katika Ukanda wa Bonde la Ufa.
"Maeneo hayo ni pamoja na Ziwa Ngozi mkoani Mbeya, Natron Manyara pamoja na Lohoi eneo lililopo Pwani‚" alisema Prof. Muhongo aliyataja maeneo hayo na kuongeza kuwa, mikoa yote iliyoko katika ukanda wa bonde la ufa.
Umeme huo utakaounganishwa katika gridi ya taifa, utasaidia kupunguza gharama za umeme huku uzalishaji ukitegemewa kuanza rasmi mwaka 2015/16.
Jitihada zote hizi zitafuata sera ya umeme ambayo imekuwepo kutoka zamani na kwamba inaendelea kufanyiwa marekebisho.
Prof. Muhongo alisema utafiti unaendelea kwa kasi na kuongeza kwamba Tanzania kama nchi yenye bonde kubwa kuliko nchi zote Afrika itaweza kuzalisha umeme mwingi.

No comments:

Post a Comment