26 July 2013

JAPAN KUJENGA UWANJA WA JUDO PEMBANa Mwajuma Juma, Zanzibar
RAIS wa Heshima wa Chama cha Judo Zanzibar, Tsuyoshi Shimaoka amesema kuwa ujenzi wa uwanja wa Judo kisiwani Pemba hautakuwa mkombozi wa Judo pekee bali na michezo mingine. Shimaoka alitoa kauli hiyo juzi mara baada ya utiaji wa saini wa ujenzi wa uwanja huo kati yake na Balozi wa Japani, Masaki Okada katika ukumbi wa Judo Amaan mjini Zanzibar, ambapo Serikali hiyo ya Japani imetoa sh. milioni 193 kusaidia ujenzi huo
.Alisema chama cha Judo kilikuwa na hamu kubwa ya kuwa na uwanja kisiwani humo ili kuweza kufanikisha ndoto zake za kuwa na viwanja vya Judo Zanzibar nzima."Ujenzi wa Budokan kisiwani Pemba hautakuwa mkombozi wa Judo pekee bali na michezo mingine pia kukamilika kwake kutakamilisha ndoto yetu ya kuwa na viwanja Zanzibar nzima," alisema. Sambamba na hilo alisema kuwa mara baada ya kukamilika ujenzi huo changamoto itakayowakabili ni kuweka samani mbalimbali pamoja na kuweka jozi za nguo za Judo na mambo mengine yanayohusu mchezo huo, ambapo vitu hivyo vitagharimu sh. milioni 200.  
Akizungumza katika hafla hiyo balozi wa Japani, Masaki Okada alisema kuwa amefurahi sana kuona kwamba michezo ya kijapani imeenea Zanzibar na hivyo kukamilika kwa ujenzi huo kutawapa fursa wanamichezo wa kisiwani humo kukuza vipaji vyao vya michezo mbalimbali ambayo itachezwa katika uwanja huo wa ndani.
Michezo mingine itakayochezwa katika uwanja huo ni pamoja na netiboli, mpira wa kikapu,Tenisi, mpira wa mikono na kareti. Kwa upande wake Waziri wa Habari Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Baraza la Michezo Zanzibar imekuwa ikichukua juhudi mbalimbali za kuimarisha michezo, lakini haiwezi kuimarika bila ya kuwepo na wafadhili.
Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kuwa ni wa miezi saba na utakamilika Januari mwakani, huku gharama za mradi mzima ukiwa ni sh.milioni 500 hadi kukamilika kwake.
.

No comments:

Post a Comment