"|Changamoto kubwa ni upungufu wa watumishi. Tulionao ni
chini ya asilimia 35 ya mahitaji ya watumishi hali ambayo inasababisha
malalamiko."
SERIKALI kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wamekuwa wakiendesha harakati mbalimbali za
kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya hususan afya ya uzazi ili kupunguza
vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua ikiwa sehemu ya Utekelezaji wa Malengo
ya Maendeleo ya Milenia (MDG).
Madhumuni ya
harakati hizo ni kupunguzwa kwa asilmia 75 kwa vifo vinavyotokana na uzazi
ifikapo mwaka 2015.Miongoni mwa mikakati inayoendelea kutekelezwa ni kupandisha
hadhi vituo vya kutoa huduma, kuhamasisha jamii juu ya afya ya uzazi, kujenga
zanahati na vituo vya afya, kuongeza idadi ya watumishi wa kada ya afya pamoja
na kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba.Hata hivyo, mratibu msaidizi wa
afya ya uzazi na mtoto katika Wilaya ya Geita, Nafka Robson, anasema kuna
changamoto kadhaa ambazo bado zinapelekea kuendelea kuwepo kwa vifo vya
wajawazito ambavyo hutokea wakati wa kujifungua.
Anasema jumla
ya wajawazito 28,012 walijifungua salama katika kipindi cha mwaka 2011 wilayani
Geita huku 18,218 kati yao wakijifungulia kwenye vituo vya tiba, 4,960
wakijifungulia majumbani na 299 wakijifungulia njiani wakati wakipelekwa kwenye
vituo vya kutoa huduma.
Mratibu
msaidizi huyo wa afya ya uzazi na mtoto katika wilaya ya Geita anasema mwaka
2011, jumla ya wajawazito 48 walipoteza maisha wilayani humo wakati wa
kujifungua, ambapo 32 walifariki wakiwa kwenye vituo vya kutoa tiba na wengine
16 walifariki katika maeneo mengine ya kijamii.
Anasema katika
mwaka 2012, jumla ya wajawazito 24,702 walijifungua salama huku idadi ya vifo
ikipungua kutoka 48 mwaka 2011 hadi vifo 34 ambavyo 30 vilitokea kwneye vituo
vya tiba na vinne vilitokea kwenye maeneo ya jamii.
Katika robo ya
kwanza ya mwaka huu, anasema jumla ya wajawazito 5,530 wamejifungua salama
katika kipindi cha kati ya Januari hadi Machi, mwaka huu, huku jumla ya vifo 14
vikitokea, ambapo 13 vilitokea katika vituo vya huduma na kimoja katika maeneo
mengine ya jamii.
Vilevile,
anaeleza kuwa vifo vingi vinasababishwa na kutokwa damu nyingi, upungufu wa
damu, maambukizi baada ya kujifungua, kifafa cha uzazi, kujitambua mapema kwa
kondo la nyuma, Ukimwi pamoja na ugonjwa wa moyo.
Anasema vifo
vya wajawazito vinaweza kupungua ikiwa wazazi watafuata maekelezo ya wataalamu
ambao pamoja na mambo mengine wanawashauri kula chakula bora kama njia ya
kuwawezesha kuwa wenye siha njema na hivyo kuzalisha damu ya kutosha.
Pia anasema
baadhi ya imani au taarifa potofu miongoni mwa jamii huchangia katika madhara
yanayoweza kuwapata wajawazito ikiwa pamoja na imani kuwa matumizi ya dawa za
Follic Acid husababisha muda wa kujifungua kuzidi miezi tisa kama ilivyo
kawaida. Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita, Dkt. Noel Makuza,
anasema serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha huduma za afya kwa wananchi,
licha ya changamoto zilizopo.
Anasema
malalamiko ya wananchi juu ya kuchelewa kupata huduma za afya katika vituo vya
umma, yanatokana na idadi ndogo ya watumishi kwani wilaya hiyo ina upungufu wa
asilimia 68 ya mahitaji ya watumishi wanaotakiwa.Dkt. Makuza anasema serikali
imeongeza watumishi wapya 70 wa afya katika mkoa mpya wa Geita, ambapo hadi
kufikia Juni 26, mwaka huu, ilikuwa imetumia zaidi ya sh.milioni 500 kununua
dawa MSD, ambao walikuwa wakiendelea kusambaza katika zahanati na vituo vya
afya vya mkoa huo.
“Kwa sasa
tatizo la dawa tumefanikiwa kulidhibiti. Hospitali ya wilaya ya Geita ina
hudumia zaidi ya watu milioni moja, idadi ambayo ni kubwa zaidi ukilinganisha
na hospitali nyingi nchini,” anasema Dkt. Makuza.
Anasema
wamenunua vitanda vipya katika hospitali ya Wilaya ya Geita pamoja na kuongeza
upatikanaji wa huduma nyingine kwa wagonjwa. Kuhusu tatizo la jenereta la
kuzalisha umeme wa akiba katika hospitali ya wilaya ya Geita, Dkt. Makuza
anasema madai hayo hayana ukweli kwani serikali imelishughulikia tatizo hilo na
kulipatia ufumbuzi baada ya kutoa jenereta mbili kwa hospitali hiyo.
Dkt. Makuza
anaongelea kuhusu vifo vya wajawazito kwenye hospitali hiyo kwa kueleza kuwa
kuna utaratibu wa kujadili malalamiko yanayotolewa na wagonjwa.
“Changamoto kubwa ni upungufu wa
watumishi. Tulionao ni chini ya asilimia 35 ya mahitaji ya watumishi hali
ambayo inasababisha malalamiko,” anasema.
Kwa kuzingatia hali hiyo Shirika
lisilokuwa la kiserikali linalojishughulisha na ubora wa huduma za afya na urahisi
wa jamii kufikiwa na huduma hizo, Tandabui Health Access Tanzania (THAT)/ Afya
redio, uliwasilia nyumbani kwa John Kisyeri (27), mkazi wa eneo la Mbugani,
kata ya Kalangalala wilayani humo.
Madhumuni ya safari hiyo ni kulenga
kupunguza vifo vya wajawazito ambapo iliamua kuzitembelea baadhi ya familia
zilizokumbwa na misiba na kutokana na akina mama kufariki wakati wa kujifungua.
“Ilikuwa asubuhi ya Mei 25, mwaka huu
wakati najiandaa kwenda kazini, mke wangu Perus Mnanka (22) alinieleza kuwa
anahisi dalili za uchungu, hivyo niende kazini kuaga ili niweze kurejea na
kumpeleka katika hospitali ya wilaya ya Geita kwa ajili ya kujifungua,” anaanza
kueleza jinsi kifo cha mkewe kilivyotokea na kuongeza:“Nilirudi nyumbani na
kumpeleka hospitali ya Wilaya ya Geita, ilikuwa saa tatu asubuhi. Kama kawaida
nilizuiliwa kuingia katika wodi ya wazazi na kuambiwa niende kutafuta chai kwa
ajili ya mjamzito”.
Anasema baada ya kupeleka chai alirudi
nyumbani kuandaa chakula cha mchana na baada ya kurudi hospitalini kupeleka
chakula hicho, alielezwa kuwa mke wake hakuwa amejifungua na kwamba alikuwa
akiendelea kupatiwa huduma.
“Hisia zangu zilinituma kuamini kwamba
kuna kitu kisichokuwa cha kawaida kinaendelea kwani nilizuiwa kuingia kumwona.
Hata simu yake ilikuwa ikiita bila majibu. Mama niliyemwacha wodini alinitaka
niendelee kuwa mvumilivu wakati huduma kwa mke wangu ikiendelea, “Niliamua
kurudi nyumbani kwa kuwa sio mbali na hospitali, ambako nilimpigia simu mama
mkwe kumjulisha juu ya kilichokuwa kikiendelea na badaye kufanya maombi ili mke
wangu ajifungue salama,” anasema mwalimu huyo wa Shule ya Sekondari Kivukoni.
Anaeleza kuwa ilipofika saa 11 jioni,
alipigiwa simu kuhitajika kufika hospitali ambako daktari alimweleza kuwa
jitihada zao za kumpatia huduma mke wake zimeshindikana na kuwa amefariki
wakati akijifungua.
“Nililia kama mtoto mdogo. Mke wangu
alikuwa na umri wa miaka 22. Ndio kwanza amemaliza shahada yake ya uhasibu.
Tulikuwa na matarajio makubwa katika maisha yetu lakini maisha yake yamefikia
kikomo. Namshukuru Mungu kwa yaliyotokea lakini najiuliza, ilikuwaje
wakashindwa kuokoa hata maisha ya kichanga?” anahoji.
U j u m b e w a h u o THAT ulimtembelea
mwalimu Kisyeri ikiwa takriban siku 21 tangu kufariki kwa mke wake, lakini
mwalimu huyo mwenyeji wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, anatupa lawama kwa
uongozi wa hospitali kutokana na uduni wa upatikananji wa huduma kwa wanawake
wanaojifungua katika hospitali ya wilaya.
“Mimi kinachoniumiza zaidi sio kifo cha
mke wangu. Najiuliza, kwanini afariki akiwa na mtoto tumboni? alihoji. Binadamu
gani anaweza kuvumilia uchungu wa uzazi kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa 11
jioni?. Nafikiri kuna uzembe katika utoaji wa huduma,” alidai mwalimu huyo.
Hali hiyo ya majonzi haimkabili mwalimu
Kisyeri pekee, mwingine ni Bahati Joseph mkazi wa eneo la Uwanja, kata ya
Kalangalala wilayani Geita, ambaye pia alidai kumpoteza mke wake Mei 24, mwaka
huu, wakati akijifungua.Joseph ambaye mke wake, Roza Sekeli alikuwa na ujauzito
wa pili, anadai kuwa alimpeleka hospitalini hapo saa nne asubuhi na kufariki
saa 12 asubuhi wakati akiwa katika harakati za kujifungua.
Hata hivyo, Joseph anadai kuwa huduma duni
inayosababishwa na upungufu wa watumishi ni sababu iliyochangia kifo cha mke
wake pamoja na mtoto aliyekuwa tumboni na kuongeza kuwa alipofika hospitalini
hapo mke wake aliongezwa maji ya uchungu ili kumsaidia kujifungua. Joseph
anasema kuwa alielezwa kuwa uchunguzi wa madaktari ulibaini kuwa mtoto
alifariki siku mbili kabla ya mama hajafikishwa hospitaini na kuwa maji ya
kuongeza uchungu aliyopewa hayakuweza kusaidia mtoto kutoka tumboni kama
ilivyokusudiwa.
“Mke wangu alikuwa akihudhuria k l i n i k
i . Mim i mwenyewe nilimsindikiza mara mbili.Ni mapenzi ya mwenyezi Mungu
lakini utajisikia vipi mzazi akipelekwa hospitali anakaa muda wote huo bila
kujifungua halafu mtoto anafia tumboni,” anahoji Joseph ambaye
anajihushughulisha na shughuli za kilimo.
Ziara hiyo pia ilifika nyumbani kwa
Freeman Kishe, mkazi wa eneo la Bomani ambaye kama ilivyo kwa wenzake, anaeleza
hisia zake kutokana na kifo cha mke wake ambacho kwa mtazamo wake kilichangiwa
na ukosefu wa umeme wa akiba katika hospitali ya wilaya ya Geita.
“Mke wangu Justina Peter, alifariki Aprili
10,mwaka huu wakati akifanyiwa upasuaji wa kurekebisha mfumo wake wa mkojo
ulioathiriwa na upasuaji uliofanyika siku 60 nyuma wakati alipofanyiwa upasuaji
baada ya kushindwa kujifungua kwa njia ya kawaida,” anasema.
Anadai umeme ulikatika wakati wa upasuaji
huo ukiendelea, ambapo jenereta haikuweza kuwashwa kwa wakati, hivyo
walishindwa kudhibiti damu kuvuja na hivyo kupelekea kifo cha mke wake. Na huko
katika kitongoji cha Bunyema, kijiji cha Bulangale kata ya Bukwimba wilaya mpya
ya Nyangh’wale mkoani Geita, familia ya Nyanjige Katoto inaendelea kusikitika
kufuatia kifo cha mtoto wao, Monica Hamis aliyefariki Aprili 3, mwaka huu,
katika kituo cha afya cha Karumwa.
Kwa mujibu wa Nyanjige Katoto, Mtoto wake
Monica ambaye alikuwa na umri wa miaka 42 na ambaye huo ulikuwa ujauzito wake
wa nane, alifariki baada ya kutokwa damu nyingi.
Changamoto iliyojitokeza katika mazungumzo
na familia hiyo ni pamoja na kuelezwa kuwa hakukuwa na kumbukukumbu sahihi za
umri wa mimba aliyekuwa nayo marehemu kwani hakuwahi kuhudhuria kliniki katika
kipindi chote cha miezi zaidi ya mitano ambacho inasadikiwa kuwa alikuwa
mjamzito.
Baadhi
ya maofisa wa THAT wakipata maelezo kutoka katika familia mojawapo iliyopatwa
na matatizo ya kupoteza ndugu kutokana na sababu za kujifungua.
No comments:
Post a Comment