WANAFUNZI 15 wa Shule ya Sekondari ya Wazazi ya Lupata
wilayani Rungwe, mkoani Mbeya wanashikiliwa na polisi kwa kosa la kuchoma moto
bweni wakipinga hatua ya wanafunzi wenzao kusimamishwa masomo kwa utovu wa
nidhamu.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Diwani Athuman, alisema tukio hilo
lilitokea Mei 14, mwaka huu saa 2.00 usiku.
Kamanda Athuman alisema kuwa
wanafunzi hao baada ya
kuona wenzao watatu wamesimamishwa masomo walianza
kufanya vurugu usiku na kuanza kuchoma moto bweni moja la wanafunzi wa kiume.
Kamanda Athuman aliwataja wanafunzi waliosimamishwa masomo kwa utovu wa nidhamu
shuleni hapo kuwa ni, Joseph Robert (18), Mwita Chacha na Daniel David (18).
“Hawa wanafunzi watatu waliosimamishwa
masomo walihamasisha wenzao kuunga mkono kupinga adhabu hiyo kwa kufanya vurugu
na kuchoma bweni hilo,”alisema Kamanda Athuman.
Alisema bweni lililochomwa moto
walikuwa wanaishi wanafunzi ambao hawakuwa tayari kuunga mkono uvunjifu huo wa
amani shuleni hapo. Aidha Kamanda Athuman alisema wanafunzi 15 wanashikiliwa na
polisi wakiwemo vinara wa fujo hizo.
Kuhusu
mali zilizoharibiwa, Kamanda huyo alisema thamani halisi ya uharibifu uliotokea
bado haijajulikana. Kamanda Athuman ametoa wito kwa jamii hasa wanafunzi kuacha
tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na badala yake
watatue matatizo kwa njia ya mazungumzo kwa kufuata mamlaka husika.
No comments:
Post a Comment