16 May 2013

Ndugu wagombea maiti mochari

Na Sophia Fundi, Karatu


 HOS P ITALI Te u l e y a Karatu wilayani hapa nusura igeuke uwanja wa masumbwi baada ya kutokea mgogoro mkubwa baina ya pande mbili zilizokuwa zikigombea maiti kuhusu eneo atakalozikwa marehemu.
Tafrani hiyo ilidumu kwa saa kadhaa mjini hapa jirani na chumba cha kuhifadhia maiti. Hali hiyo ilitokea baada ya mume wa marehemu, Bw. Sauli Zakaria, kutaka kwenda kumzika mke wake, Eliza Mathayo, nyumbani kwao mkoani Mtwara.
Hata hivyo ndugu wa marehemu waligoma wakihoji iweje
azikwe mbali na nyumba yake waliyokuwa wakiishi. Wakizungumza na gazeti hili, ndugu wa marehemu walisema hawakubaliani na ndugu yao kuzikwa mbali (mkoani Mtwara) kwani ndugu zake wengine hawataweza kwenda kushiriki mazishi.
Akizungumza kwa njia ya simu baada ya ndugu hao kuzuia maiti hiyo, iliyokuwa isafirishwe jana saa nane mchana kwenda Mtwara, mume wa marehemu, Bw. Zakaria alisema yeye kama mume wa marehemu ndiye ana mamlaka ya kupanga ni wapi azikwe mke wake.
Alisema anashangazwa na ndugu hao kukataa asimzike mke wake ambaye walimpa akiwa hai na kufunga naye ndoa halali. “Leo hii wananikatalia nisimzike ninakotaka... mimi naamua kuwaachia maiti yao na mimi nitaondoka na watoto wangu,”alisema Bw. Zakaria na kuongeza;
“Nimeamua kuwaachia maiti yao hivyo naishia zangu na watoto wangu, wamzike mtu wao.” Baada ya malumbano hayo yaliyochukua muda mrefu, Bw. Zakaria aliwashukuru majirani waliokuwa wamekusanyika nyumbani kwake na kuwataka kutawanyika kwani msiba hautakuwepo katika eneo hilo.
Baada ya kutoa kauli hiyo alifunga mlango wa nyumba yake na kwenda kusikojulikana huku akiacha maiti ya mke wake hospitali kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.
Alipoulizwa kuhusiana na hali hiyo Katibu wa Hospitali hiyo, Bi. Joyce Kajivo, alisema kuwa wao kama viongozi wa hospitali wanasubiri maamuzi ya mume wa marehemu kwani yeye ndiye mwenye maamuzi ya wapi amzike mke wake na taratibu zote za hospitali zimekamilika.

1 comment: