16 May 2013

Mbunge aibana Serikali utekelezaji wa bajeti

Na Goodluck Hongo


 MBUNGE wa Fuoni kwa tiketi ya CCM, Bw.Said Mussa Zuberi, ameshangazwa na wabunge kupitisha bajeti za wizara mbalimbali, lakini fedha hizo hazipelekwi kama zinavyoidhinishwa.
Alitoa kauli hiyo mjini Dodoma wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2013/2014. Alisema inashangaza wabunge kupitisha bajeti, lakini fedha zinazotolewa ni kidogo na vilevile hazipelekwi zote kwenye wizara husika.
 Alitolea mfano mradi wa Kurasini jijini Dar es Salaam, ambapo zilitakiwa zitolewe zaidi ya sh. bilioni
120 kwa ajili ya mradi huo, lakini ni kiasi cha sh.bilioni 10 ndizo zilizotolewa na Serikali.
“Kama kwe l i t u n a t a k a kutengeneza ajira kwa kusaidia vijana zaidi ya 100,000, kwa nini bunge likipitisha bajeti ya Wizara fedha hazipelekwi zote?”Alihoji Bw. Zuberi.
Alibainisha kuwa mradi huo wa Kurasini ambapo Wachina wangewekeza zaidi ya sh.bilioni 60 unashindikana hadi leo kutokana na Wizara kutopewa fedha zote kama ilivyoomba katika bajeti iliyopita, ambapo watu wengi wangepata ajira.
Alishangazwa na kitendo cha bunge hilo kutenga muda kidogo kuchangia bajeti ya wizara hiyo wakati hiyo ndiyo wizara muhimu kwani ndiyo inatoa ajira kupitia viwanda.
Naye Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Bw. Nimrod Mkono, alisema hawezi kuunga mkono hoja ya bajeti ya wizara hiyo hadi pale atakapopata majibu kutoka kwa Waziri, Dkt.Abdalaah Kigoda, kuhusiana na matatizo ya wizara hiyo.
Alisema ofisi ya Brela imeoza na haifai kuendelea kutoa huduma hizo, kwani hata ofisini haina viti wala meza, majalada yamejaa na yametunzwa holela hadi karibu na chooni.
Alisema mtu anachukua miaka kati ya miwili hadi mitatu ndipo apate usajili. “Ofisi ya Brela imeoza nakuomba waziri fumua hii na kuisuka upya kwa mazingira hayo hataweza kufanya biashara kwa hali hii, kwani wizara hii ina matatizo makubwa lakini hawa Brela wanafanya nini kwa kweli siungi mkono hoja hadi nipate majibu ndiyo nitaunga mkono hoja,” alisema Bw. Mkono
Naye Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya CHADEMA Mchungaji Peter Msigwa, alisema wamachinga nchini wamekuwa wakipigwa mabomu badala ya wahusika kukaa chini na kutafuta njia ya kutatua matatizo yao.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2013/2014 Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Kigoda aliliomba bunge kupitisha kiasi cha zaidi ya sh.bilioni 108 kwa mwaka wa fedha ujao ili Wizara iweze kutekeleza majukumu yake.
Alisema sh. bilioni 29 zitatumika katika matumizi ya kawaida, sh. bilioni 22 kulipa mishahara na sh. bilioni 78 kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment