WANACHAMA 331 wa Umoja wa Wauza Mitumba wa soko la
Mchikichini (MIMCO)wameanza kupewa viwanja kwa kila mwanachama wa umoja huo ili
wajenge nyumba za kuishi.
Viwanja hivyo walivyopewa wanachama
wameuziwa na umoja wao wa MIMCO baada kununua shamba zaidi ya heka 20 eneo la
Pemba Mnazi Wilayani Temeke,ambapo kila mwanachama hulipia sh.milioni 1.2
pamoja na kupatiwa leseni ya kiwanja kilichopimwa na Serikali.
Akisoma taarifa ya Bodi ya MIMCO
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Bw.
Ajali Mohamed alisema kila mwanachama hai wa umoja
huo ambaye hadaiwi ada atapatiwa eneo la kujenga.
Alisema kila mwanachama atagawiwa
eneo la kujenga baada kukamilisha taratibu na fedha atalipa kwa awamu tofauti
kwa kuanzia sh. 400,000.
"Madhumuni ya wanachama wangu
kuwagawia kila mmoja kiwanja ni ili wajenge nyumba za kuishi watoke katika
nyumba za kupanga halafu waweze kupata mikopo kwa urahisi kutokana dhamana ya
leseni zao," alisema Bw. Mohamed.
Bw.Mohamed alisema umoja huo
ulianzishwa mwaka 2005 mwezi Mei kikiwa na wanachama 331 kati yao wanawake 24
wanaume 307 na wajumbe wanane wa bodi hiyo.
Aliwataka wanachama wa umoja huo kulipa ada
kila mwaka ili umoja huo uweze kukua sambamba na kukuza hisa zao.
Pia bodi hiyo imependekeza viwanja hivyo
wauziwe wanachama walio hai ambao hawadaiwi hisa wala ada na mtu atakayepewa
kiwanja alipe pesa ndani ya miezi mitatu ili waweze kupata fedha kwa maendeleo
ya MIMCO na wanachama wake.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mstaafu wa soko
la Mchikichini Bw. Deo Mkali, aliwataka wanachama wa MIMCO wachague viongozi
bora na si bora viongozi ili chama hicho kisipoteze mwelekeo katika uongozi
wake.
Bw.Mkali alisema chama hicho kinapofanya
chaguzi zake kichague viongozi bora na wenye upeo katika utendaji ambao
watasaidia chama kupiga hatua zaidi katika elimu ya ujasiriamali.
Pia alikitaka chama hicho kiwape
kipaumbele wanawake kuwa sehemu ya uongozi wa bodi na viwanja vigawiwe pasipo
dhana ya ubaguzi.
"Nimestaafu kwa hiari yangu ila
natoa wosia kwa chama tujiepushe na wanachama wanaojitokeza kuleta vurugu na
uchochezi sokoni kwa ujumla pamoja na kujiepusha na masuala ya udini, siasa
ukabila na ubaguzi vinavyoashiria kujitokeza sokoni kwa sasa,"alisema
Bw.Mkali.
No comments:
Post a Comment