WAFANYABIASHARA
wa mazao ya nafaka na wasafirishaji wenye magari malori, wilayani Kahama
wameandamana hadi ofisi za Halmashauri ya wilaya wakipinga ushuru wanaotozwa
kuwa ni mkubwa.
Wafanyabiashara
hao waliandamana juzi na kuvamia ofisi za halmashauri hiyo baada ya malori
yaliyokuwa yamebeba nafaka kukamatwa na askari mgambo kutokana na mgogoro huo
wakipinga kutozwa ushuru mara mbili.
Kundi hilo la
wafanyabiashara wakiwa katika ofisi za Halmashauri hiyo, askari mgambo
aliyekuwa akilinda alilazamika kupambana nao bila mafanikio huku akitishia
kuwalipua kwa bunduki hali iliyowatia hasira na kusababisha vurugu kubwa.
Wakiongea na waandishi katika ofisi
hizo wafanyabishara hao walikuwa
wakipinga kutozwa ushuru mara mbili wa sh.
2,500 kwa kila gunia la mahindi na mpunga wanapoyasafirisha toka vijijini kwa
wakulima.
Bw. Imani alisema wao kama
wafanyabiashara wamekuwa wakilipa ushuru wa sh.500 kwa kila gunia kwa mzabuni
wa halmashauri wanaponunua toka kwa wakulima wanapoanza kuyasafirisha na
wamekuwa wakitozwa tena sh. 2,000 hali, ambayo wanapinga.
Mgogoro huo wa ushuru unatokana na
kutofautiana katika kikao cha hivi karibuni cha baraza la madiwani na watendaji
wa halmashauri, ambapo madiwani walipendekeza ushuru wa mazao uwe sh.1,000 kwa
gunia, lakini mkurugenzi alisema wao wamepitisha shilingi 2000.
Katika kikao hicho diwani wa kata ya
Lunguya Bw. Benedicto Manwali aliwasilisha pendekezo la Madiwani la kutoza
ushuru wa mazao msimu huu sh.1000, lakini lilikataliwa na mkurugenzi, Bi.
Isabella Chilumba katika kikao hicho hali iliyopelekea kubaki hivyo hivyo.
Aidha kutokana na mvutano huo ndiyo
uliopelekea kuzusha mgogoro huo wa ushuru,ambapo Bw.Manwali alipotafutwa
aliitupia lawama Halmashauri kuwa imesababisha hali kutokana na kupinga
mapendekezo ya ushuru walioupitisha katika kikao cha ndani cha madiwani wa CCM.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama,
Bw. Joseph Gwassa akiongea na wafanyabiashara hao ambao walishinda katika ofisi
hizo kutwa nzima alisema suala la mgogoro huo hawezi akalitolea uamuzi peke
yake mpaka atakapolifikisha katika vikao vinavyohusika.
No comments:
Post a Comment