27 May 2013

Mndolwa awataka wananchi kujikita katika kilimo cha alizeti

Na Mwandishi Wetu, Korogwe


 MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (MNEC) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Tanga, Dkt. Edmund Mndolwa amewataka wananchi wakazi wa Wilaya ya Korogwe Vijijini kujikita katika kilimo cha alizeti ili kiweze kuwakomboa kiuchumi.
Dkt. Mndolwa alieleza kuwa mazingira ya wilaya hiyo na Mkoa wa Tanga kwa ujumla yanahimili kilimo cha alizeti hivyo kama wananchi watakithamini na kulifanya zao hilo kuwa la biashara watanufaika haraka kwa kuondokana na umaskini na utegemezi.
Kiongozi huyo aliyasema hayo wakati akiwahamasisha wananchi kutoka vijiji vya kata na tarafa za wilaya hiyo juzi na kuwahakikishia wananchi hao kwamba kilimo cha alizeti hakitawaacha maskini kutokana na utafiti wa kisayansi kuthibitisha ubora na manufaa ya zao hilo ikiwa ni
pamoja na kuthibitika kuwa na soko kubwa.
"Kwa vile chama chetu kinahimiza kilimo kwanza, katika ilani chini ya Mwenyekiti na Rais wetu, Dkt. Jakaya Kikwete, Kamati Kuu ilipitisha uamuzi wa kuwa alizeti ni zao la biashara katika wilaya yetu na mimi nimeagizwa na chama kuhimiza zao hili ili muweze kunufaika nalo.
"Lakini kabla ya kufikia hatua hii ilinibidi nitembelee Kata ya Kwadelo, Kondoa mkoani Dodoma ambayo ni ya mfano hapa nchini kwa kilimo hicho ili kujifunza namna ya kulima zao hilo hivyo limeni zao hili ambalo kwa wilaya yetu tutanufaika zaidi kuliko Kondoa, ambao wanategemea msimu mmoja wa mvua tofauti na sisi tunaopata misimu miwili," alieleza.
Akifafanua manufaa makubwa ya zao hilo, Dkt. Mndolwa alisema kuwa hekari moja inaweza kutoa magunia 12 hadi 18 na kwa maana hiyo wastani wa hekari moja unaweza kupata lita 300 za mafuta ambazo ni sawa na thamani ya sh.450,000.
Pia alisema kuwa mkulima akiamua kulima misimu yote miwili kutokana na hali ya hewa ya wilaya hiyo, atakuwa na uhakika wa kuingiza sh.900,000 kwa hekari, pato ambalo litawasaidia kupata mahitaji nuhimu ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto na huduma za afya na malazi kwa familia.
Dkt. Mndolwa alisema mafuta ya zao hilo ndiyo yenye soko kubwa kwa sasa, hivyo kuwataka wananchi hao kutokuwa na wasiwasi juu ya upatikanaji wa soko na badala yake waunge mkono kilimo hicho ili kiweze kuwakomboa kiuchumi.
Katika kuonyesha kwamba anataka wananchi hao walime alizeti, Dkt. Mndolwa aliahidi kuwalimia vijana ekari tano kila kata, ambao watajiunga katika vikundi vya watu watano ili kuanza kupata shamba darasa.
Akitilia mkazo juu ya umuhimu wa kilimo hicho, Diwani wa Kata ya Kwadelo, Kondoa, mkoani Dodoma, Alhaji Omari Kariati alisema kuwa wakati wananchi wa kata yake wanaanza kulima zao hilo hawakuanza na mafanikio ya moja kwa moja lakini kwa sasa wamefanikiwa.
"Kwa sasa mkulima mdogo katika kata yangu analima ekari 50 na kuna watu wanalima mpaka ekari 200, kitu ambacho kimefanya wananchi wa Kata ya Kwadelo kutokuwa na shida ya fedha badala yake wanashindana kimaendeleo.
"Hata vijana na akina mama mkiamua mnaweza kwani katika kata yetu, kundi lenu ndilo lenye kumiliki uchumi mkubwa na hawana muda wa kupoteza zaidi ya kuzungumzia namna ya kuboresha kilimo chao cha alizeti, kitu ambacho mnatakiwa kukifanya pia watu wa Korogwe Vijijiji," alieleza.
Kariati alisema wakati wanaanza kulima, kata yake ilikuwa na matrekta matano lakini kutokana na manufaa makubwa ya kilimo hicho kata ina matrekta 65, ambayo yanamilikiwa na wananchi wenyewe.

No comments:

Post a Comment