19 May 2013

Viongozi wa kijiji wanao chochea chuki, mauaji kukamatwa

Na Sammy Kisika, Sumbawanga


 SERIKALI wilayani Sumbawanga imeweka mikakati ya kuanza kuwachukulia hatua kali za kisheria kwa kuwakamata viongozi wa vijiji wote ambao wamekuwa wakishiriki katika kuchochea chuki na kushiriki katika vitendo vya mauaji yanayotokana na imani za kishirikina.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Mathew Sadoyeka katika ziara yake anayoendelea kuifanya kwenye vijiji na kata mbalimbali wilayani humo kwa lengo la kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Msandamuungano jana, Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa vitendo vya mauaji ya imani za kishirikina vimekuwa vikiongezeka wilayani humo katika
miaka ya karibuni ikiwa ni pamoja na matukio ya wananchi kuchomewa moto nyumba zao kutokana na imani hizo.
“Kipindi cha mwezi Juni mwaka jana jumla ya wananchi 24 waliuawa kutokana na matukio ya imani za kishirikina, je, ikitokea hivyo kwa kipindi cha mwaka mzima itakuwaje, hii hali si ya kuvumiliwa lazima tuchukue hatua,”alisema Sadoyeka.
Alisema baada ya kukaa na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo amebaini kuwa vitendo vingi vya mauaji vinavyotokea kwenye vijiji vimekuwa vikiwahusisha viongozi wa vijiji hivyo ambao wamekuwa wakifahamu mipango yote ya kuuawa kwa watu wanaotuhumiwa kwa uchawi, lakini viongozi hao wamekuwa wakikaa kimya hadi matukio hayo yanapotokea.
“Hawa viongozi wamekuwa na tabia ya kuwasiliana na vikundi ambavyo vinafanya vitendo hivyo, lakini kabla ya mauaji hayajafanyika hujifanya kusafiri na kuja hapa mjini kisha baada ya tukio wanakuja hapa ofisini na kudai kuwa tukio hilo limetendeka wakati wao hawapo kwenye maeneo yao ya utawala kumbe alikuwa anafahamu mipango yote,”alisema Sadoyeka.

No comments:

Post a Comment