19 May 2013

TBC kukagua mabati,vifaa vya maji

Na Grace Ndossa


 SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS)limesema kuwa kwa sasa wanahamia kukagua mabati na vifaa vya maji kutokana na kukithiri kwa bidhaa zisizo na viwango hapa nchini.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu Bw. Joseph Masikitiko wakati walipokutana na wafanyabiashara wa nondo pamoja na wamiliki wa viwanda hivyo kwa ajili ya kuwapatia elimu kuhusu namna ya kuzalisha bidhaa zenye ubora na kupunguza bidhaa hafifu.
Alisema kuwa hii ni kutokana na wafanyabiashara wengi kuzalisha bidhaa zisizo na vuwango na kuchanganya na zenye viwango kwa kuwauzia wateja.
Bw.Masikitiko alisema kuwa ukaguzi huo ni endelevu watakagua kila kiwanda kuhakikisha inapunguza bidhaa hafifu hapa nchini.
Alisema wafanyabiashara pamoja na wamiliki wa viwanda kutoka Dar es Salaam na
Arusha wamehudhuria mafunzo hayo na kujadili namna gani ya kuboresha bidhaa zao ziwe na viwango vya kimataifa.
Hata hivyo, alisema kuwa tangu walipoanza kukagua nondo wameweza kukamata tani 500 kwenye viwanda mbalimbali na wanataraji wiki ijayo kuziharibu nondo hizo kwani hazifai kwa matumizi ya ujenzi.
"Tumetoa tangazo kwenye vyombo vya habari ambapo tulitoa muda wa mwezi mmoja wafanyabiashara wote wazalishaji wa bidhaa zilizo na viwango vya lazima wajisajili na TBS waweze kukaguliwa pamoja na kupatiwa mafunzo kama hawatafanya hivyo watatozwa faini ya sh milioni 50 hadi 100,"alisema Bw. Masikitiko.
Alisema kuwa tangu tutoe tangazo hilo imebaki wiki moja, hivyo kwa mfanyabiashara mwenye bidhaa za viwango vya lazima ambavyo vinaathiri moja kwa moja kwa mtumiaji mfano kama nondo, mabati nyaya za umeme na vifaa vingine atatozwa faini au kifungo.
Hata hivyo, alisema kuwa ni vyema mzalishaji mwenye leseni kuzingatia masharti yaliyomo kwenye leseni yake pamoja na kuzalisha bidhaa inayokidhi viwango vinginevyo atafutiwa leseni ya alama ya ubora.

No comments:

Post a Comment