KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Shinyanga, Mberito Magova,
ameliponda Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kudai linastahili
kuvunjwa, kuitisha uchaguzi upya kwa sababu linamuaibisha Rais Jakaya Kikwete.
Alionesha
kukerwa na kitendo cha Serikali ya CCM kutumia takwimu zisizo sahihi kuonesha
uchumi unakua wakati unaporomoka kwa kasi ya kutisha.
Magova ambaye
hivi karibuni alistaafu katika nafasi ya Katibu wa CCM Wilaya, aliyasema hayo
juzi mjini humo alipokuwa akizungumza na gazeti hili juu ya mustakabali wa
Taifa kwa sasa na kudai kuwa, wabunge wameshindwa kuisimamia Serikali badala
yake wanatanguliza itikadi za vyama.
Alisema matukio
yanayotokea ndani ya Bunge kwa sasa, inaonesha ni jinsi gani wabunge
wasivyoelewa wajibu wao wanapokuwa katika vikao hivyo, kuacha kujadili mambo
muhimu yenye masilahi kwa Taifa badala yake wanatumia fursa walizonazo
kutukanana.
“Wabunge wetu
wameshindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu, mfumo wa uendeshaji wa Serikali
haufuatwi matokeo yake kila jambo linabaki kumtegemea rais wa nchi.
“Utakuta mbunge
anasimama na kuhoji Serikali imelifanyia nini jimbo lake...kauli hii kutolewa
na mbunge ni kosa, Waziri Mkuu kama kiongozi wa Serikali bungeni, ndiye
anayepaswa kumhoji mbunge ana mipango gani ya maendeleo katika jimbo lake ili
Serikali ichukue hatua ya kuitekeleza.
“Mbunge
anasimama bungeni na kulalamikia mdondoko wa elimu jimboni kwake wakati yeye
hajawahi hata siku moja kuitisha kikao cha bodi za shule ili kuangalia ni jinsi
gani watakabiliana na changamoto zilizopo,” alisema.
Aliongeza kuwa,
hivi karibuni Mbunge wa Bariadi Mashariki, mkoani humo, Bw. John Cheyo (UDP),
alisimama bungeni na kumshauri Rais Kikwete alivunje Bunge kwa vile limepoteza
mwelekeo wakati yeye ndiye aliyepaswa kuonesha mfano kwa kujiuzulu ubunge wake.
“Kama kauli
yake ilikuwa na dhamira ya kweli, angeanza kujiuzulu yeye...alichokisema ni
mwendelezo wa siasa za majukwaani ili kujizolea umaarufu kwa jamii,” alisema.Kuporomoka
kwa uchumi.
Akizungumzia kauli inayotolewa na Serikali mara kwa mara juu ya uchumi
wa nchi kukua, Magova alisema kauli hiyo si ya kweli kutokana na uhalisia wa
maisha ya Watanzania wengi pamoja na mzigo mkubwa wa madeni yaliyopo.
Alisema kama
unakua ni wazi maisha ya Watanzania yangekuwa bora kuliko ilivyo sasa mbapo
sehemu kubwa ya wananchi kutwa wanashindia mlo mmoja na kipato chini ya dola
moja kwa siku.
“Anayesema
uchumi wetu unakua ni muongo, huenda anatumia takwimu za upimaji uchumi ambazo
si sahihi, deni la Taifa ni kubwa kiasi cha kutisha, hali ya maisha ni mbaya
tofauti na miaka 40 iliyopita,” alisema Magova.
Aliongeza
kuwa, ushahidi mwingine wa kuporomoka kwa uchumi wa nchi ni kufa kwa viwanda
vingi vikubwa ambavyo vilianzishwa katika utawala wa Serikali ya Awamu ya
Kwanza ambapo hivi sasa kila kitu kinaendeshwa na wawekezaji.
No comments:
Post a Comment