19 May 2013

Ngumi Ridhaa Mwanza watimuana

Na Daud Magesa, Mwanza


 CHAMA cha Ngumi za Ridhaa Mkoa wa Mwanza (MBA) kimekumbwa na mgogoro baada ya Katibu Mkuu,Meja Mstaafu Michael Changarawe, kumsimamisha Mwenyekiti wa muda, Kapteni mstaafu,Annasery Mkiwa.
Mgogoro huo wa kutimuana umekuja siku chache baada ya Kapteni Mkiwa, kuwafukuza Meja Changarawe na mchumi mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Madeleke,akiwatuhumu kuchakachua bajeti ya kufanikisha mashindano ya Majiji kutoka sh.milioni 33 hadi sh.milioni 62.
Katibu huyo kwenye barua yake ya kumsimamisha uongozi mwenyekiti huyo wa muda yenye Kumb.Na.MBA/ADM/VOL.-2/14/15 anaeleza kuwa,wamemsimamisha baada ya
kuwafukuza kwenye ofisi aliyowakabidhi waitumie kwa shughuli za maandalizi ya michuano ya ngumi.
Alisema kuwa, amechukua uamuzi mgumu kwa sababu wako kwenye maandalizi ya kupokea timu za Majiji ya Afrika Mashariki, zitakazoshiriki mashindano ya ngumi yanayotarajiwa kufanyika jijini Mwanza hivi karibuni.
"Nasema ni uamuzi mgumu kwa sababu ndicho kipindi ambacho nilikuwa nahitaji umoja wenu kuliko wakati mwingine wowote ule.Sasa jana (juzi) ulitusambaratisha na nikatoka kichwa chini.Vinginevyo utuombe radhi kwa kosa ulilotenda kinyume na ahadi yako kwa vyombo vya habari," alisema Meja Changarawe katika barua hiyo ya Mei Mosi mwaka huu.
Kwa Upande wake Kapteni Mkiwa, alikiri kuwafukuza Meja Changarawe na Madeleke, akiwatuhumu kutaka kumhusisha kwenye utapeli wa fedha za serikali na wafadhili baada ya kuongeza fedha zaidi kwenye bajeti iliyopangwa,hivyo asingeweza kufanya kazi nao.
Mkiwa alisema kabla ya kusimamishwa alimtaarifu Katibu huyo wa MBA kuwa asingeweza kuendelea kukaimu nafasi ya Uenyekiti wa chama hicho kwa sababu ya uteuzi wake kutotambuliwa na chombo chochote katika Wilaya ya Nyamagana na mkoa mzima.
"Niliwaambia waondoke na siwezi kufanya kazi nao kwa vile walitaka kunihusisha na utapeli wa fedha za serikali na wafadhili.Niliona kuna mambo ambayo hayatekelezeki kuhusu ufunguzi na ufungaji wa mashindano na mialiko ya Marais, Jakaya Kikwete na Uhuru Kenyatta,"
"Pia nilipinga ongezeko la sh.milioni 29 kuwa halina mantiki.Mabondia kulazwa DVN Hosteli na kula kwa mama ntilie ni kufuja fedha sababu nijilitolea kambi iwekwe chuoni kwangu MICTAT wapikiwe na wafanyakazi wangu bila malipo, sisi MBA tununue chakula na matumizi tu," ilisema barua hiyo ya Mkiwa kwenda kwa Katibu Mkuu wa MBA.
Aidha, Kapteni Mkiwa alisema,Meja Changarawe anaonesha jamii kuwa anaendesha chama hicho kama mali yake baada ya kueleza kuwa angeshirikisha vyama vya wilaya ya Nyamagana na Mkoa wa Mwanza kwenye uchaguzi wa Taifa bila kufanya uchaguzi wa vyama hivyo katika ngazi husika.

No comments:

Post a Comment