ASKARI wawili wa Jeshi la Polisi akiwemo mmoja wa
Kikosi cha Usalama Barabarani, Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, wamelazwa
katika Hospitali ya Nyangao, baada ya pikipiki waliyokuwa wakiitumia kugongana
na gari ndogo.
Ajali hiyo ilitokea wakati askari
hao wakimkimbiza mwendesha pikipiki aliyekuwa amekiuka Sheria za Usalama
Barabarani. Kamanda wa Polisi mkoani humo, George Mwakajinga, alisema ajali
hiyo imetokea wilayani humo Mei 20 mwaka huu.
Aliwataja askari hao kuwa ni F 6986
PC Living aliyevunjika miguu yote miwili na mkono wa kushoto na G 2116 PC
Edwin, ambaye amepata maumivu ya ndani kwa ndani.
“Hawa askari walikuwa kazini wakiwa
wamepakiana kwenye pikipiki aina ya
Suzuki namba PT 2951, iliyokuwa
ikiendeshwa na PC Living, waligongana na gari ndogo aina ya Land Cruiser namba
T 398 AME iliyokuwa ikiendeshwa na Bw. Juma Mandundu.
“Ajali hii ilikuwa mbaya na dereva
wa gari amejisalimisha mwenyewe Kituo cha Polisi Wilaya ya Nachingwea na
atafikishwa mahakamani baada ya taratibu kukamilika,” alisema.
Mashuhuda wa ajali hiyo, wameliambia
gazeti hili kuwa, askari hao walikuwa wakiikimbiza pikipiki nyingine ambayo
dereva wake alikaidi amri ya kumtaka asimame na kuelekea upande wa Barabara ya
Masasi.
Walisema
kitendo hicho kiliwafanya askari hao wachukue pikipiki yao na kuanza kumfukuza
na walipofika katikati waligongana uso kwa uso na gari ndogo ambalo hawakuliona
kutokana na vumbi.
No comments:
Post a Comment