JESHI
la Polisi nchini, limeendelea kuwasaka wachochezi wanaotumia simu za mkononi
kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno (sms), ili kuhamasisha vurugu.
Operesheni hiyo inafanywa na Kikosi Maalum kutoka Makao Makuu ambao
wanasaidiana na Makamanda wa Polisi kwenye mikoa mbalimbali nchini pamoja na
wananchi.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es
Salaam jana na Msemaji wa jeshi hilo nchini, SSP Advera Senso, alisema tayari
jeshi hilo limemkamata mtu mwingine mkoani Lindi kwa kuhusika na uhalifu wa
aina hiyo.
“Tayari tumekamilisha upelelezi na
kukusanya ushahidi wa mtu aliyekamatwa Dar es Salaam kwa tuhuma za kutuma
meseji za uchochezi na leo atafikishwa mahakamani.
“Tunaendelea kukamilisha ukusanyaji
ushahidi dhidi ya wanaofadhili ambao
wanashawishi vitendo hivi ili na wao
waweze kufikishwa mahakamani mapema,” alisema.
Aliwashukuru wananchi kwa
ushirikiano wao wa kutoa taarifa zinazofanikisha operesheni hiyo na kuomba
waendelee kuwaunga mkono kwa kutoa taarifa za watu wanaofadhili vitendo vya
uhalifu kwa njia ya pesa au ushauri.
SSP
Senso alitoa onyo kwa mtu yeyote au kikundi cha watu wanaojihusisha na vitendo
vya uchochezi kuacha mara moja kwani watakamatwa bila kujali vyeo vyao au
umaarufu wao.
No comments:
Post a Comment