BARAZA la Habari nchini (MCT), limesema
halitatetereka kupigania haki za waandishi wa habari badala yake wataendelea
kusimamia weledi, maadili na maendeleo ya kitaaluma kupitia programu
mbalimbali.
Katibu Mtendaji wa MCT, Bw. Kajubi
Mukajanga, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa
habari wakati akitoa ufafanuzi wa kauli iliyotolewa na Mbunge wa Kondoa Kusini,
Bw. Juma Nkamia (CCM), kuwa baraza hilo na Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), ni
taasisi NGOs zenye masilahi binafsi.
Bw. Nkamia
alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma hivi karibuni wakati akichangia mjadala
wa Bajeti ya Wizara Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Kutokana na
kauli hiyo, Bw. Mukajanga alisema baraza hilo limesikitishwa
na kauli hiyo
yenye lengo la kukwamisha kazi zao kwa uhuru.
“Kauli hii ina
nia mbaya kwa ustawi wa baraza huru ambalo limefanikiwa sana katika Kanda ya
Afrika, MCT haipo tayari kuona kazi nzuri iliyofanywa kwa miongo miwili
ikanyagwe, kuupuzwa na watu wachache.
“Historia ya
Baraza inajieleza yenyewe kwani lilianzishwa na wanahabari wenyewe mwaka 1995
baada ya kupinga mpango wa Serikali iliyotaka kuweka sheria mbaya ya kudhibiti
vyombo vya habari,” alisema Bw. Mukajanga.
Alisema wakati
Bw. Nkamia akiwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya
Jamii, aliongoza ujumbe wa wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar, kwenye ziara ya mafunzo nchini India mwaka 2011.
Aliongeza kuwa,
safari hiyo iliandaliwa na MCT ili wabunge na wawakilishi waende kujifunza
jinsi Sheria ya Haki ya Kupata Habari ilivyokuwa inafanya kazi.
“Katika
safari hile, Bw. Nkamia aliongea mambo mazuri kuhusu jitihada za wadau wa
habari; iweje leo hii awe msaliti, tunaomba kauli yake iliyojaa dharau
ipuuzwe,” alisema.
No comments:
Post a Comment