27 May 2013

Dkt. Salim ahimiza maadili kwa viongozi, Watanzania


Na Mwandishi Wetu,
Zanzibar


 WA Z I R I Mk u u Ms t a a f u , Dk t . S a l im A hme d Salimu, amewataka viongozi na Watanzania kwa ujumla kuzingatia maadili kwani taifa limefika hapa lilipo kutokana na ukosefu wa maadili kwa viongozi na wananchi kwa ujumla.
Kutokana na hali hiyo, alitoa mwito kwa viongozi na Watanzania kwa ujumla, kuzingatia maadili ya uongozi na kwa Watanzania kuzingatia maadili ya utaifa alioacha mwasisi wa Taifa hili, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Dkt. Salim, aliyasema hayo, katika mahojiano maalum mara baada ya uzinduzi wa Tawi jipya la Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere uliofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, eneo la Bububu, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, mwishoni mwa wiki.
Alisema hatua hiyo itasaidia kulinda misingi mikuu ya taifa letu ambayo ni
umoja, usawa, amani na utulivu ambayo sasa imeanza kumomonyoka.
Alikuwa akijibu swali kuhusu hali ya Taifa letu katika kuzienzi tunu za taifa letu za umoja, usawa, amani na utulivu alizoacha Mwalimu Nyerere.
Akichangia suala hilo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, alisema viongozi wengi kwa sasa hawafuati misingi ya uongozi aliotuachia Mwalimu Nyerere.
Alitolea mfano malumbano ya kidini yanayotokea hivi sasa, kuwa ni uthibitisho wa kuanza kupotea kwa misingi ya umoja aliyoacha Mwalimu Nyerere.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Mwalimu Nyerere, Dkt. Chinuno Magoti, amesema, kwa kutambua umuhimu wa falsafa ya Mwalimu Nyerere kuhusu usawa, umoja, amani na utulivu, chuo hicho cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, kinatoa mafunzo kwa vitendo.
Alisema kamwe hauwezi kusikia migomo yoyote katika chuo hicho kutokana na kufundisha utii na nidhamu ya hali ya juu.
Tawi jipya la Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, lilizinduliwa rasmi eneo la Bububu mjini Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, mwishoni mwa wiki.

No comments:

Post a Comment