CHAMA
cha Wananchi (CUF), kimesema kitaendelea kuwalaani kwa nguvu zote watu
wanaotaka kuwagawa Watanzania, wawe ni viongozi au wananchi kwa misingi ya dini
zao.
Taarifa
iliyotolewa na chama hicho kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilisema
hivi karibuni gazeti moja (si Majira), liliandika habari iliyomhusisha
Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba na masuala ya udini.
Katika
taarifa hiyo, CUF kimeitaka Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo,
kutovifumbia macho baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vinataka kuwapeleka
Watanzania kusiko hasa kipindi hiki ambacho nchi imegubikwa na matukio mengi
yanayohusu migongano ya
dini na kusababisha uharibifu katika nyumba za ibada.
“Tunasisitiza na kulaani uandishi wa
aina hii, tutaendelea kulaani wale wanaolenga kuwagawa Watanzania wawe ni
viongozi au wananchi kwa misingi ya dini zao,” ilisisitiza taarifa hiyo.
Chama hicho kiliongeza kuwa, magazeti
ya aina hiyo yamekuwa yakichochea uhasama wa kidini na kuwabagua wananchi kwa
mujibu wa imani zao yakihusishwa na uchochezi huo na baadhi ya vyama vya
kisiasa pamoja na viongozi wake.
“Tumeshangazwa na tuhuma za udini
kuelekezwa kwa Mwenyekiti wetu Taifa...hii inaonesha uandikaji habari wa aina
hii una lengo la kuvigawa vyama vya siasa kwa falsafa ya udini,” iliongeza
taarifa hiyo.
Kimesema hali halisi ya habari hiyo ni
kutaka kuonesha kwa wananchi kuwa Prof. Lipumba na Rais Jakaya Kikwete kila
mmoja akiwa ni Mwenyekiti wa chama cha siasa, waligubikwa na imani za udini
katika kampeni zao kwa kutegemea kura za Waislamu.
Taarifa hiyo ilisema kuwa, habari hiyo
ilikwenda mbali zaidi na kusema kuwa, “Prof. Lipumba amekuwa akitumia misikiti
na viongozi wa dini hiyo ili Waislamu nchini waendelee kukiunga mkono chama
chake hasa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Chama chetu hakiwezi kumzuia Prof.
Lipumba, asihudhurie ibada katika msikiti wowote anaotaka, kualikwa kanisani au
kwenye mahekalu ya Kihindu,” ilisema taarifa hiyo.
Iliongeza kuwa, CUF kinatambua kuwa
Prof. Lipumba ni Muislamu hivyo chama hakiwezi kumzuia asihudhurie ibada kwenye
Msikiti na sehemu nyingine ambazo ataalikwa na kutakiwa kutoa hotoba kwa
waumini au waliomualika.
“Kumbukumbu zinaonesha Rais wa Awamu ya
Tatu, Bw. Benjamin Mkapa wakati akiwa madarakani alitangaza kuwapa Waislamu
Chuo cha Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kilichopo mkoani Morogoro na kuwa
Chuo Kikuu cha Kiislamu.
“Si vibaya
kwa Prof. Ibrahim Lipumba kutoa kauli ya kuwataka Waislamu wajipange katika
ibada aliyoalikwa,” ilifafanua taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment