16 May 2013

Denmark yashauri utoaji misamaha ya kodi

Grace Ndossa na Mariam Mziwanda


 NAIBU Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Kitaifa wa Serikali ya Denmark, Bw. Charlotte Slett, ameshauri Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ihakikishe malengo ya misamaha ya kodi yanapunguza umaskini na kuleta usawa katika jamii. Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Naibu waziri huyo, alipotembelea Mamlaka hiyo kujua mipango ya miaka mitano iliyowekwa kuhakikisha inapunguza umaskini Tanzania. Alisema Serikali ya Denmark inahakikisha misamaha ya kodi ni
asilimia hamsini kwa hamsini, ambayo haiwaumizi wananchi wake. Hata hivyo alisema Serikali ya Denmark inasaidia Tanzania kila mwaka kwa dola milioni 80 na kwamba watakutana na waziri wa fedha kuangalia ni namna gani wanaweza kusaidia bajeti ya wizara yake. Naye Kamishna Mkuu TRA, Bw. Harry Kitillya, alisema misamaha ya kodi inatolewa kama mtu akikosa sababu za msingi zinazofanya asamehewe au kupunguziwa kodi. Wakati huo huo TRA imezindua awamu ya pili utekelezaji wa mradi wa Mashine za kielektroniki ambayo imelenga kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani. Hayo yalibainishwa jana na Naibu Kamishna MKuu wa Mamlaka hiyo Bw. Rished Bade, alipokuwa anazindua mashine hiyo na kueleza kuwa awamu hiyo imelenga kuanza na kundi la wafanyabiashara 200,000. Alisema matumizi ya mfumo huo kwa miaka miwili ya utekelezaji yameonesha mafanikio katika ukuaji wa makusanyo yatokanayo kodi.

No comments:

Post a Comment