19 May 2013

DC Ludewa aapa kutowasaidia wananchi watakaokumbwa na njaa


Na Nickson Mahundi, Ludewa
MKUU wa wilaya ya Ludewa, Bw.Juma Madaha ameapa kutowasaidia wananchi wilayani humo watakaokumbwa na balaa la njaa kutokana na wananchi hao kuanza kuvuna mahindi na kuyauza kwa bei rahisi na kusahau kuacha akiba ya baadaye.
Bw.Madaha alisema takwimu inaonesha kuwa mtu mzima moja ndani ya mwaka anatumia gunia tano za mahindi kwa chakula lakini baadhi ya wananchi huyauza mahindi yote kutokana na uroho wa fedha hali ambayo husababisha familia kuhangaika zinapokosa chakula na kuilaumu Serikali.
Alisema wilaya ya Ludewa kwa mwaka 2013 imeweza kupata mvua za kutosha kutokana na hali hiyo hakuna kijiji wala kata ambacho kina upungufu wa chakula itashangaza kama kuna familia zimeanza
kuuza mazao na kutoacha akiba.
Aidha amewataka watendaji wa vijiji kulisimamia hilo na hatapokea taarifa yoyote ya kijiji wala kata itakayotaka chakula cha msaada kwa mwaka huu na mwaka ujao kutokana na wilaya hiyo, wananchi wake kujitosheleza kwa chakula kama hakitatumiwa vibaya.
Sitaomba chakula cha msaada kutoka Serikalini kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa wilaya yangu ni bora nikafukuzwa kazi kwani mahindi yako yakutosha na anayeanza kuvuna na kuyauza kwa bei rahisi bila kuacha akiba shauri yake na serikali haitalaumiwa kwa hilo," alisema Bw.Madaha.
Bw.Madaha aliwataka wakulima kuacha mara moja tabia ya kupokea fedha kwa wanunuzi wa mahindi kabla hayajavunwa kwani kuna wachuuzi hupita na kugawa fedha mapema ili waweze kujipatia mahindi hayo kwa bei rahisi msimu wa mavuno.
Naye Diwani wa kata ya Ludewa Bi.Monica Mchilo alisema imeshazoeleka kwa wananchi wa wilaya hiyo kuuza mazao yote na kushindwa hata chakula cha ziada hali inayosababisha serikali kulaumiwa kwa kutozisaidia baadhi ya kata zenye tabia hiyo.
Bi.Mchilo aliwataka wananchi wenye tabia kama hiyo kuacha mara moja kwani serikali iko kwa ajili ya kusaidia maeneo ambayo mvua hazikunyesha na si maeneo kama Ludewa ambako mvua zimenyesha na mazao yamekubali lakini wananchi wanayauza bila ya kuacha akiba.
Alisema wilaya ya Ludewa ni kati ya wilaya nyingi nchini zenye rutuba ya kutosha na inastawisha aina nyingi ya mazao; hivyo itakuwa aibu kama Serikali itaombwa chakula cha msaada wakati kila kitu kinapatikana; uzembe ni utunzaji tu.
Tutatia aibu kwa taifa kama tutaomba chakula cha msaada wakati tuna kila kitu ninachowaomba wananchi wenzangu ni kuacha tabia ya kuanza kupukucha mahindi na kuyauza mapema namna hii kwani thamani ya mahindi inapanda siku hadi siku tukiyatunza" alisema Bi.Mchilo.
Bi.Mchilo amewataka kunzia ngazi ya kaya kuanza kulindana kwa kukemea tabia ya kuuza chakula chote bila ya kuacha akiba kutokana na hali halisi ya wilaya hiyo kupokea wageni wa migodini.

No comments:

Post a Comment