02 April 2013

Wakristo waondolewe hofu la usalama wao kanisani kwa vitendo


LEO Wakristo wote duniani, wanaadhimisha kifo cha
Yesu Kristo aliyeteswa msalabani mjini Yerusalemu.

Siku ya leo ni mwanzo wa Sikukuu ya Pasaka ambayo Yesu
Kristo alifufuka maada ya mateso yaliyosababisha kifo chake msalabani ambapo Wakristo huitumia siku hiyo kushangilia
ushindi wa kufufuka kwake na ukombozi wao.


Hivi karibuni, Jeshi la Polisi nchini liliwaonya baadhi ya watu waliosambaza vipeperushi vya kutaka kufanya vurugu katika
ibada ya Pasaka kwenye makanisa mbalimbali nchini.

Tishio hilo bado linaendelea kusumbua mioyo ya waumini ambao leo, wanashiriki ibada ya kufa kwa Yesu Kristo katika makanisa mbalimbali mbali ya polisi kuwahakikishia usalama wao.

Msemaji wa jeshi hilo nchini, Bi. Advera Senso, alisema wamejipanga kuimarisha usalama wa raia, mali zao katika
kipindi chote cha sikukuu.

Lengo ni kuwataka Wakristo washeherekee sikukuu hiyo kwa
amani na utulivu hivyo ulinzi huo, utaanzia katika nyumba za
ibada na maeneo mbalimbali ya starehe ili kuhakikisha hakuna vitendo au viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.

Jeshi hilo linakiri kuwa, uzoefu unaonesha baadhi ya watu hutumia kipindi cha sikukuu kufanya matukio ya uhalifu kutokana na mikusanyiko ya wananchi katika maeneo mbalimbali.

Sisi tunasema kuwa, tamko la Jeshi la Polisi kwa waumini ambao
leo wanaanza mchakato wa kufikia kilele cha Sikukuu ya Pasaka liwe kwa vitendo ili kuwaondolea hofu waliyonayo.

Kama itatokea leo baadhi ya makanisa yamevamiwa katika ibada
ya Ijumaa Kuu na baadhi ya waumini kujeruhiwa, tamko la polisi linaweza kuwaweka katika mazingira magumu ya kuaminiwa na wananchi hivyo kusababisha utendaji kazi kuwa mgumu.

Imani yetu ni kwamba, waumini wataamini kile wanachoambiwa
kwa kuona si kwa mdogo hivyo upo umuhimu wa jeshi hilo, kutembea juu ya maneno yake kwa kuweka askari tena wenye
silaha katika nyumba zote za ibada.

Hali hiyo itawapa moyo waumini kushiriki ibada ya Pasaka bila wasiwasi wa kuhofia usalama wa maisha yao kama ilivyo sasa
ambapo matukio ya hivi karibuni dhidi ya viongozi wa dini,
bado yanaendelea kusumbua mioyo yao.

Ni vyema Jeshi la Polisi likaweka askari maalumu (makachero), ambao watazunguka mitaani ili kuwapa ulinzi waumini ambao wengi wao hutembea kwa miguu tena kwenye vikundi kwenda
katika nyumba za ibada na wakati wa kurudi.

No comments:

Post a Comment