02 April 2013

Katibu aliyefukuzwa CCM arudishwa kundini


Na Suleiman Abeid, Shinyanga

HATIMAYE Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Shinyanga Mjini, Bw. Charles Shigino, aliyekuwa amesimamishwa uongozi, amerejeshwa katika nafasi yake.

Bw. Shigino alisimamishwa uongozi akidaiwa kugoma kwenda kuhojiwa kwenye Kikao cha Kamati ya Maadili Wilaya ambapo
juzi alikabidhiwa barua rasmi ya kurejeshwa katika nafasi yake
yenye namba CCM/SHY/MJN/U.30/2/63.

Akizungumza na gazeti hili, Bw. Shigino alielezea kuridhishwa kwake na uamuzi huo na kuongeza kuwa, umetolewa kwa kuzingatia haki kwani uamuzi wa kumsimamisha ulikuwa haujzingatia Katiba na kanuni za CCM bali ni shinikizo la watu wachache.

Barua hiyo ambayo ilisainiwa na Katibu wa CCM Shinyanga
Mjini, Bw. Charles Charles, ilikuwa na kichwa cha habati ambacho kinasema “Kuendelea na shughuli za uongozi wa Chama”.

“Utaendelea na shughuli zako za kila siku za Katibu wa Siasa na Uenezi ambazo zimeainishwa katika ibara ya 87 (a) – (f) ya Katiba ya CCM inayotumika sasa,” ilisema barua hiyo.

Akizungumzia uamuzi wa kurudishwa katika nafasi yake, Bw. Shigino alisema daima atahakikisha anafanya kazi zake kwa kuzingatia Katiba, kanuni na taratibu za chama hicho.


Alisema mazingira ya sasa kisiasa nchini, yanahitaji mshikamano
wa dhati miongoni mwa wana CCM ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania kuhakikisha kila kiongozi anasimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama chao.

“Bila umoja na mshikamano miongoni mwa viongozi na wanachama kwa ujumla, ipo hatari ya wapinzani kupata mwanya wa kujipatia umaarufu nchini...hali hii inaweza kuleta matokeo banaya kwa chama chaetu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015,” alisema.

Wiki iliyopita, Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, ilimsimamisha uongozi Bw. Shigino kwa kile kilichodaiwa kukaidi kuhudhuria Kikao cha Kamati ya Maadili aweze kuhojiwa kutokana na tuhuma mbalimbali alizokuwa akituhumiwa kuzifanya kinyume cha katiba ya chama hicho.

No comments:

Post a Comment