05 April 2013

Stanbic yadaiwa fidia bil. 3/- kwa kufunga duka Kariakoo



Na Rehema Mohamed

BENKI ya Stanbic Dar es Salaam, imefunguliwa kesi ya madai na Kampuni ya Star Digital Technology & Pritways Limited na Oliver's Investment & Co (1993) Limited, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ikidaiwa fidia ya sh. bilioni 3, baada ya kufunga duka la kampuni hiyo lililopo Mtaa wa Pemba na Sikukuu, Kariakoo.


Kesi hiyo namba 11 ya mwaka 2013, ipo mbele ya Jaji Mwaikugile wa mahakama hiyo ambapo Aprili 2 mwaka huu, ilisikilizwa upande wa madai na mahakama hiyo kutoa amri ya wadaiwa kufungua duka hilo mara moja.

Mbali na benki hiyo, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Kampuni ya Marcas Investment & Co na Fodeys Security & Alarm System wanaodaiwa kufunga duka hilo.

Kwa mujibu wa hati ya madai, kampuni hizo zinaidai benki ya Stanbic fedha hizo kama fidia inayotokana na hasara ya kutofanya biashara tangu duka hilo lifungwe Mach 15 mwaka huu, ambapo
kila kampuni inadai fidia ya sh. bilioni 1.5.

Madai mengine ni wateja wao kukosa huduma, kudhalilishwa, kupunguza uaminifu kwa wateja, jamii na kukosa kipato ambapo
kesi hiyo itaendelea kusikilizwa Aprili 25 mwaka huu.

Habari kutoka nje ya mahakama, Mkurugenzi wa Kampuni ya Star Digital Technology & Pritways Limited, Bw. Oliver Limwangu, alisema pamoja na Mahakama Kuu kuiamuru benki hiyo ifungue
duka hilo, hadi sasa bado haijafanya hivyo.

Bw. Limwangu alisema, benki hiyo inaonekana kupingana na
amri hiyo ambayo ilitolewa Aprili 2 mwaka huu, mbele ya
wakili wao.

Wakili wa benki hiyo Bw. Pasco Kanala, alisema wameshindwa kufungua duka hilo kwa sababu mahakama haijawapelekea nakala
ya amri iliyotolewa Aprili 2 mwaka huu.

“Mahakama ikituletea nakala ya amri hii tutalifungua lakini bado hatujaipata wala wadaiwa wengine ambao ni mawakala wa benki
hii,” alisema Bw. Kanala.

Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Ilala, imetoa amri ya zuio kwa kampuni ya Vijay Auto Works Ltd na Super Auto Mart la kuuza yadi namba 48 eneo la Viwandani Mbagara.

Amri hiyo ya zuio ilitolewa mahakamani hapo na Hakimu Mushi  wa mahakama hiyo Machi 27 mwaka huu, ambapo yadi hiyo inamilikiwa na kampuni ya Kiswele Salt Works Ltd na Mtumwa Binti Kiswele Complex Ltd.

Zuio hilo limetokana na kufunguliwa kwa shauri la madai namba 9/2013 dhidi ya walalamikiwa ambao ni kampuni ya Vijay Auto Works Ltd na Super Auto Mart ambazo zinataka kuuza yadi hiyo kwa madai ya kuidai kampuni ya Kiswele Salt Works Ltd na Mtumwa Binti Kiswele Complex Ltd.

Katika shauri hilo, Kiswele Salt Works Ltd na Mtumwa Binti Kiswele Complex Ltd, inadai fidia ya sh. milioni 88,320,000
ambazo ni gharama za maumivu ya kutangazwa katika mabango
na magazetini kuwa zinadaiwa na kampuni hizo.

No comments:

Post a Comment