02 April 2013

Polisi Moro waibania Yanga *Azam FC yainyuka Ruvu Shooting



Na Eliza Mayemba, Morogoro

VINARA wa Ligi Kuu ya Vodacom, Yanga jana walibanwa mbavu na Polisi Morogoro baada ya kulazimishwa suluhu katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.


Kwa matokeo hayo Yanga imeendelea kukalia usukani wa ligi hiyo na pointi 49, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 43 huku Simba ni ya tatu kufikisha pointi 35. 

Katika mechi hiyo Polisi iliingia kwa nguvu na kufanya shambulizi kali langoni mwa Yanga, dakika ya kwanza ambapo, Nicholas Kabipe kuachia shuti lililodakwa na kipa Ally Mustafa 'Bathez'.

Yanga nayo ilicharuka ambapo dakika ya 26, Nadir Haoub 'Canavaro' alikosa bao la wazi baada ya kushindwa kupiga kichwa mpira wa kona iliyochongwa na David Luhende.

Hata hivyo hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, hakuna iliyokuwa imepata bao.

Kipindi cha pili Yanga, ilifanya mabadiliko ambapo Nizar Khalifan na Said Bahanuzi walitoka na nafasi zao kuchukuliwa na Stephano Mwasyika na Didier Kavumbagu.

Dakika ya 61, Polisi ilikosa bao baada ya Mokili Rambo kushindwa kuunganisha krosi safi iliyochongwa na Kibipe.

Katika mechi hiyo Polisi walionekana kukamia, lakini hadi kipenga cha mwisho kinapilizwa hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.

Naye Omari Mngindo, anaripoti kutoka Mlandizi kuwa Azam FC jana iliendelea kutakaka katika michuano hiyo baada ya kuicha Ruvu Shooting bao 1-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Mabatini.

Bao la Azam lilifungwa na Kipre Tchetche kwa shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni.

No comments:

Post a Comment