05 April 2013

Jambazi akutwa na risasi 1,276 za SMG


Na Mwajabu Kigaza, Kigoma

JESHI la Polisi mkoani Kigoma, limemkamata mkazi wa Kijiji
cha Kitambuka, Kata ya Mnanila, Wilaya ya Buhingwe, mkoani
Kigoma Bw. Mwanzo Wilson (45), ambaye inadaiwa ni jambazi
sugu akiwa na risasi 1,276 za bunduki aina ya SMG alizozihifadhi katika dumu lenye mafuta ya Mawese akitaka kuzisafirisha.


Kamanda wa Polisi mkoani humo, Frasser Kashai, alisema mtuhumiwa alikamatwa Aprili 2 mwaka huu, saa 12 jioni, katika   eneo la Shule ya Msingi Mhalulo, Kijiji cha Kitambuka.

Alisema mtuhumiwa huyo amekamatwa kutokana na taarifa zilizotolewa na raia ambapo jeshi hilo lilifanya msako katika
kijiji hicho ambacho kinasifika kwa biashara ya risasi na
bunduki kutoka nchi jirani ya Burundi.

Bw. Julius Magige ambaye anakaimu nafasi ya upelelezi mkoani humo, alisema kuwa mtuhumiwa ni miongoni mwa majambazi
sugu wanaoshiriki matukio mbalimbali ya uhalifu.

Alisema mtuhumiwa alihusika katika tukio la uporaji fedha katika Benki ya CRDB, Tawi la Temeke, Dar es Salaam miaka miwili iliyopita na kukaa Gereza la Ukonga.

“Licha ya mtuhumiwa kufungwa Tanzania, pia alihukumiwa kifungo nchini Burundi kutokana na makosa mbalimbali ya uhalifu hivyo ni mtu hatari katika maeneo mbalimbali.

“Katika mbao za matangazo za polisi kuna picha yake aliyopigwa nchini Burundi akiwa mahabusu, pia kuna picha tatu za majambazi kati yao mmoja amefariki miaka mingi iliyopita na wawili wapo
hai akiwemo mtuhumiwa,” alisema Bw. Magige.

Alisema atafikishwa mahakamani baada ya kukamilika
upelelezi wa awali ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

3 comments:

  1. picha za majambazi kama hawa ni muhimu kuzipost ili tuwajue

    ReplyDelete
  2. ATAKAA SIKU MBILI GEREZENI KISHA WATAMTOA, LKN ANGELIKMATWA KAIBA MAYAI YA KUKU ANGELIKAA GEREZANI AKAJISAHAU HUKO.

    ReplyDelete
  3. JAMAA HUYU NI HATARI SANA, SISI WAKAZI WA MANYOVU (KASULU) HATA SALAMU KWAKE TULISHAHAMISHA! TATIZO LA NCHI YETU, JAMAA ATAKAA GEREZANI MUDA TU THEN MUNAMUONA NJE! PAMOJA NA MLOLONGO HUU WA MATUKIO...WATAKWAMBIA "UCHUNGUZI" UNAENDELEA!!!

    ReplyDelete