02 April 2013

Askofu: Viongozi hawana uzalendo *Malasusa aibana serikali kuanguka kwa ghorofa Dar *Waumini watakiwa kudumisha amani, mshikamano



Na Waandishi Wetu

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dkt. Alex Malasusa, amesema tukio la kuporomoka ghorofa 16 mwishoni mwa wiki
Dar es Salaam ni matokeo ya usimamizi mbovu wa majengo.

Alisema katika tukio hilo ambalo limegharimu maisha ya watu,
maelekezo ya kitaalamu hayakufuatwa hivyo ni fundisho kwa
Serikali kuhakikisha ajali za aina hiyo zinaepukika.

Dkt. Malasusa aliyasema hayo jana katika Ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front, Dar es Salaam.

“Kilichotokea mwishoni mwa wiki ni jambo la kusikitisha, tukio
hili liwe mwanzo wa utawala kubadilika...ajali nyingi zinaweza kuzuilika kama taratibu za ujenzi zitafuatwa na kusimamiwa
ipaswavyo na watu wenye dhamana,” alisema.

Alisema hivi sasa, si wakati wa kunyoosheana vidole au kulauimiana kwani msiba huo unawahusu Watanzania wote.

Akizungumzia Sikukuu ya Pasaka, alisema siku hiyo ni muhimu kwa Wakristo wote ambapo Yesu Kristo amefufuka baada ya kifo chake kilichotokana na mateso ili kuwakomboa wanadamu.

Jimbo la Mbinga

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga, mkoani Ruvuma, John Ndimbo, alisema tukio la kuporomoka
ghorofa 16 jijini Dares Salaam ni matokeo ya baadhi ya viongozi kukosa hofu ya Mungu na uzalendo wa nchi yao.

Alisema wapo baadhi ya viongozi ambao wamekosa uzalendo katika utendaji kazi wao hivyo kusababisha matatizo na maafa kwenye jamii.

Askofu Ndimbo aliyasema hayo jan katika ibada ya mkesha wa Pasaka iliyofanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Kiriani na kuwataka waumini wa kanisa hilo kuwaombea watu wenye
shida mbalimbali wakiwemo majeruhi wa tukio hilo na
familia za marehemu waliopoteza maisha.

Askofu Isack Amani

Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi, mkoani Kilimanjaro, Mhashamu Isack Amani, amewataka waumini wa kanisa hilo, kumuombea Papa Francis I, aliyechaguliwa katika nafasi hiyo
hivi karibuni ili Mwenyezi Mungu ampe nguvu, hekima na
busara katika kutekeleza majukumu yake.

Alisema maombi hayo yatamsaidia kiongozi huyo kuwa na afya njema na kuifanya kazi ya kanisa kwa mafanikio makubwa.

Askofu Amani aliyasema hayo mjini Moshi jana wakati akitoa salamu zake kwa waumini wa kanisa hilo katika Ibada ya Pasaka iliyofanyika Kanisa Kuu la Kristu Mfalme.

Aliwashukuru waumini wa kanisa hilo kwa kumuombea Hayati Amedeus Msarikie aliyekuwa Askofu mstaafu wa jimbo hilo
wakati wa ugonjwa wake na kutoa ushirikiano mkubwa katika
mazishi yake baada ya kufariki dunia Februari mwaka huu,
mjini Nairobi, nchini Kenya.

Wakati huo huo, Askofu Amani, alitoa wito kwa wazazi kujenga tabia ya kukaa na watoto wao ili kuwapa maadili mema kwani hivi sasa maadili ya vijana wengi nchini yameanza kuporomoka.

"Vijana wengi hawana maadili mema tena, hatuhitaji uchunguzi kujua hili bali nawaomba wazazi make na watoto wenu hasa katika kipindi hiki cha likizo ya Pasaka na kuwakumbusha maadili mema kama ilivyokuwa zamani,” alisema Askofu Amani.

Aliongeza kuwa, ushirikina, usuria, (nyumba ndogo), uchawi na ulevi wa kupindukia ni changamoto kubwa kwa waumini na jamii
hivyo umefika wakati wa kila mtu kumrudia Mwenyezi Mungu.

“Hatuna budi kuingia katika undani wa amani yetu ili tuweze kuiboresha, hatuwezi kujiimarishsa wenyewe, hivyo tumuombe Mwenyezi Mungu atuimarishe maana yeye habahatishi,” alisema.

Askofu Dallu

Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Geita, Damian Dallu, ameitaka Serikali kukomesha vitendo vya uchomaji makanisa
na vitisho kwa viongozi viongozi wa dini ya Kikristo ili
kujenga amani ya nchi.

Askofu Dallu aliyasema hayo katika ibada ya mkesha wa Sikukuu
ya Pasaka iliyofanyika Kanisa Kuu mjini Geita na kusisitiza kuwa,  vitendo vya uchomaji makanisa na vitisho kwa viongozi wa dini
vinapaswa kukemewa na kila mtu wakiwemo viongozi wa Serikali na kama vitaachwa, vitachangia kuchafua amani ya nchi.

“Tumefikia hatua ya kusali kwa shaka na wasiwasi mkubwa, hii si ishara njema kwa nchi yetu ambayo imekuwa iikisifiwa na mataifa mengine duniani kwa kuwa na amani, upendo, maelewano na mshikamano imara,” alisema Askofu Dallu.

Aliitaka Serikali kuchukua hatua stahiki kwa vikundi vinavyotaka kuvuruga amani ya nchi na kuwasihi waumini, kuacha tabia ya kuitumia Sikukuu ya Pasaka kutenda maovu kwani kufanya
hivyo ni kumchukiza Mungu.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu Kanisa la African Inland (AICT), Jimbo la Geita, Mussa Magwesela, alisema vitendo vya uchomaji makanisa vinavyofanywa na baadhi ya watu nchini, vinawaumiza
Wakristo na kuitakla Serikali ichukue hatua bila kusita.

Alisema Serikali ina jukumu la kuhakikisha amani na usalama
wa wananchi unadumishwa kwa kuwakamata wahusika wa uhalifu huo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Kudumisha amani

Katika kuadhimisha Sikukuu ya Pasaka, waumini wa Kanisa Katoliki nchini, wametakiwa kudumisha amani na upendo
kwa watu wote bila kujali itikadi imani zao.

Paroko wa kanisa hilo Parokia ya Mtakatifu Stephano Shahidi Nyasubi, lililopo mjini Kahama, mkoani Shinyanga, Padri Donasian Mbuya, alisema aliyasema hayo jana katika Ibada ya Pasaka na kuongeza kuwa, waumini wanapoadhimisha siku hiyo lazima waoneshe upendo bila kubagua mtu kwa itikadi ya dini.

“Ndugu zagu waumini, tusichoke kumuomba Mungu aendelee kuilinda amani tuliyonayo ili wanaotaka kuichezea washindwe,
lazima Watanzania tuilinde amani yetu kwa maombi,” alisema.

Rais mstaafu Mkapa

Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamini Mkapa, amewataka Watanzania kutokubali kutenganishwa kwa
misingi ya udini.

Mkapa aliyasema hayo jana Mjini Masasi, mkoani Mtwara, katika Ibada ya Pasaka iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki la Masasi baada ya waumini kumuomba atoe neno la baraka.

Alisema Watanzania wanapaswa kupinga masuala yote ya kubaguana na kuwakemea watu wanaohatarisha amani ya
nchi kwa misingi ya udini.

Akizungumzia Katiba Mpya, Bw. Mkapa alisema italeta muelekeo mzuri wa misingi ya kuabudu kwani kila mtu ana haki ya kuabudu vile anavyoona inafaa kwa upande wake.

Katika hatua nyingine, Bw. Mkapa aliwataka Watanzazia kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuongoza si kuangalia itikadi za vyama vyao vya siasa.

Aliwataka wakazi wa Masasi kufanya kazi kwa bidii na kuacha
tabia ya kuilaumu Serikali panapotokea kasoro mbalimbali.

Mhashamu Nyaisonga

Askofu wa Jimbo Katoliki Dodoma, Mhashamu Gervas Nyaisonga, amani ya nchi imeanza kuchezewa jambo ambalo Watanzania hawapaswi kuruhusu hali hiyo ienndelee.

Alisema inasikitisha hivi sasa baadhi ya viongozi wanazungumzia masuala ya udini, fitina na chuki jambo ambalo linaweza kuliweka Taifa mahli pabaya na kusababisha machafuko.

Ulinzi makanisani

Jeshi la Polisi nchini, jana liliweka ulinzi mkali katika makanisa mbalimbali ili kutoa fursa kwa waumini wa dini ya Kikristo kushiriki ibada ya mkesha wa Pasaka kwa amani na utulivu.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika baadhi ya makanisa
jijini Dar es Salaam, ulibaini jeshi hilo lilitekeleza tamko la kuimarisha ulinzi katika nyumba za ibada.

Kamanisa yaliyotembelewa ni Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph,
Azania Front, Kanisa Katoliki Chang'ombe na Msimbazi ambapo
polisi walionekana wakilanda nje makanisa wakiwa na silaha
baadhi yao wakiwa na sare wengine kiraia.

Imeandikwa na Grace Ndossa, Goodluck Hongo, Joseph Mwambije, Eliasa Ally, Heckton Chuwa, Patrick Mabula, Faida Muyomba, Pendo Mtibuche, Cornel Anthony na Rachel Balama.


























No comments:

Post a Comment