02 April 2013

Tukipuuza ya Lowassa, majengo mengi yataua na kuundwa tume



TUKIO la kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu 36, majeruhi 17, limeibua maswali mengi kwa wananchi wa kada mbalimbali.

Baadhi ya viongozi wa dini, nao hawakusita kuelezea hisia zao
juu ya uzembe wa baadhi ya watendaji waliopewa dhamana ya kukagua ubora wa majengo yaliyo kwenye ujenzi.


Taarifa ya Meya wa Manispaa ya Ilala, Bw. Jerry Silaa kudai Mkandarasi na mmiliki wa jengo walijichukulia uamuzi wa
kuongeza ghorofa sita badala ya 10 kwa mujibu wa kibali
walichopewa, nayo imeibua maswali mengi.

Wapo wanaosema uundwaji wa tume yanapotokea majanga mbalimbali ni utamaduni ambao tumeanza kuuzoea kwa sababu Serikali imeshindwa kuyafanyia kazi majibu ya tume husika.

Hivi karibuni, Waziri Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli, mkoani Arusha, Bw. Edward Lowassa, alitoa ushauri wake
kupitia gazeti moja linalotoka kila siku (si Majira), juu ya
hatua za kuchungua ili maghorofa yasiendelee kuanguka.

Katika maelezo yake, Bw. Lowassa alisema, upo umuhimu wa Serikali kuifanyia kazi ripoti ya uchunguzi aliyoiunda mwaka
2006 wakati huo akiwa Waziri Mkuu.

Aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu, kuifanyia kazi ripoti ya kitaalamu iliyochunguza ubora wa maghorofa jijini Dar es Salaam ili kuepuka majanga ya aina hiyo mara kwa mara ambapo ripoti hiyo ilibaini zaidi ya majengo 100 yamejengwa chini ya kiwango.

Sisi tunaungana na ushauri wa Bw. Lowassa kuitaka Serikali ifanyie kazi ripoti hiyo ili Taifa lisiingie kwenye aibu ya kukosa uwajibikaji dhidi ya watendaji wasiojua wajibu wao, kupoteza maisha ya Watanzania wasio na ongezeko la yatima.

Ongezeko la idadi ya majengo yanayoendelea kuanguka nchini, yanaiweka nchi yetu katika wakati mgumu kimataifa hasa kwa kuzingatia kuwa, taarifa za matukio hayo huripotiwa kwenye
vyombo mbalimbali vya habari duniani.

Jiji la Dar es Salaam limezungukwa na maghorofa mengi ambayo kimsingi, ujenzi wake umefanyika kinyume na taratibu lakini hakuna hatua zozote ambazo Serikali imezichukua ili kudhibiti hali hiyo.

Kama tutaendelea na uzembe wa kutosimamia sheria zilizopo, idadi kubwa ya Watanzania watapoteza maisha kuliko idadi ya waliokufa katika tukio hili hivyo ni wajibu wa Serikali kuzingatia hilo.

Maendeleo tunayoyataka katikati ya jiji si wingi wa majengo
kama uyoga ambayo ujenzi wake haufuati taratibu wala kutoa
nafasi ya eneo la kupaki magari na kupumzika.

Tume ziundwe kuchunguza matukio yanayotokea lakini kama majibu ya tume husika hayafanyiwi kazi ni sawa na kuwaangamiza Watanzania waliotoa ushirikiano kwa tume husika na ushauri wa nini kifanyike ili kuepuka majanga mbalimbali.

No comments:

Post a Comment