11 March 2013

Serikali yataka uangalizi maalum kwa watuhumiwa.Na Rehema Mohamed

SERIKALI imewasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kutaka watu wanne wanaotuhumiwa kukutwa na nyaraka za uchochezi, wawe chini ya uangalizi maalumu.


Watu hao ni Bw. Shehe Zuberi, Bw. Basoty Tandalah, Bw. Mohammed Sharif na Bw. Salum Mohambi.

Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo jana na wakili wa Serikali Bw. Benard Kongola, mbele ya Hakimu Emilius Muchauru aliyekuwa akisikiliza maombi hayo.

Kwa mujibu wa Bw. Kongola, alisema Serikali inaomba watu hao wawe chini ya uangalizi kwa muda ambao mahakama itaona unafaa ambapo maombi hayo yaliwasilishwa kwa hati ya kiapo iliyoapwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi Hamisi Mhaka.

Kamishna Mhaka alidai kuwa, watu hao walikutwa na nyaraka mbalimbali zinazohusika na uchochezi katika jamii kwa ajili ya kutenda makosa zikiumiza imani za dini nyingine.

Kutokana na hali hiyo, aliiomba mahakama hiyo wajibu maombi
ili watu hao wadhaminiwe na wadhamini wanaoweza kutimiza masharti ya dhamana na mahakama iwawekee amri yoyote itakayoona inafaa.

Hakimu Muchauru alisema, kilichowasilishwa mahakamani si mashtaka bali ni maombi yaliyoambatana na kutoa masharti ya dhamana kwamba, kila mmoja awe na wadhamini wawili ambao
wote pamoja na mjibu maombi (walalamikiwa), watasaini
dhamana ya shilingi milioni tano.

Alisema wadhamini wawe wafanyakazi wa Serikali au taasisi inayotambulika pia wajibu maombi wanatakiwa kuingia mkataba
wa kuwa na tabia njema kwa mwaka mmoja na kuripoti Kituo
cha Polisi Kati.

Aliwaeleza wajibu maombi kuwa, kwa miezi mitatu ya kwanza watatakiwa kuripoti mara mbili kila mwezi kituoni hapo na baada
ya hapo wataripoti mara moja kila mwezi na miezi sita iliyobakia mara moja na hawatakiwi kutoka nje ya Dare s Salaam bila kibali cha polisi wa kituo hicho.

Wajibu maombi wote walishindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo walirudishwa rumande hadi Machi 18 mwaka huu kwa ajili
ya shauri hilo kutajwa.

No comments:

Post a Comment