05 March 2013Na Grace Ndossa

MAHAKAMA ya Rufaa nchini, jana imetupilia mbali ombi la Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura ya DOWANS, kutaka Shirika la Umeme nchini (TANESCO), liilipe zaidi ya sh.
bilioni 122, kwa kuvunja mkataba kinyume cha sheria.

Katika ombi hilo, DOWANS inapinga pingamizi ambalo liliwasilishwa na TANESCO baada ya Mahakama Kuu
kukubali kusajili uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa
ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC).

ICC iliitaka TANESCO iilipe DOWANS fedha hizo kama
fidia ya kuvunja mkataba wa biashara kinyume cha sheria.

Kampuni ya DOWANS inadai kuwa, kwa mujibu wa kanuni za Mahakama ya Rufaa, pingamizi hilo lilipaswa kuwasilishwa ndani ya siku 60 tangu kutolewa hukumu lakini iliwasilishwa baada ya muda huo hivyo waliomba ombi hilo litupwe kwa gharama.

Hata hivyo, TANESCO kupitia Wakili wake Bw. Richard Rweyongeza, alidai walichelewa kuwasilisha pingamizi hilo kwa sababu Mahakama Kuu ilichelewa kuwapa nakala ya hukumu na  mwenendo wa kesi ambazo ni nyaraka zinazotakiwa kuambatanishwa wakati wa kukata rufaa.

Alidai waliandika barua kwa Msajili wa Mahakama hiyo kuomba nyaraka hizo, lakini hadi jana walikuwa hawajapata.

Akisoma uamuzi uliotolewa na jopo la Majaji Steven Bwana, Benard Luanda na Edward Rutakangwa ambaye ndiye Mwenyekiti wa jopo hilo, Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Bi. Ester Mkwiza, alisema ombi la TANESCO liliwasilishwa ndani ya muda unaostahili.

Alisema TANESCO hawakuwa na wajibu wa kumkumbusha Msajili kuwapa nyaraka zinazohitajika katika kuwasilisha rufaa yao pia hakuna ushahidi wowote unaoonesha shirika hilo lilipewa nyaraka hizo kama inavyodaiwa na DOWANS.

Aliongeza kuwa, kutokana na sababu hizo, anatupilia mbali
ombi la DOWANS.

Katika hukumu iliyotolewa na ICC, Novemba 15,2011, TANESCO iliamriwa kuilipa kampuni hiyo zaidi ya dola za Marekani milioni 65, riba na gharama za kuendesha kesi baada ya kuvunja mkataba kinyume cha sheria.

Hata hivyo, shirika hilo lilipinga hukumu hiyo ambapo Septemba 28,2012, Jaji Emilian Mushi wa Mahakama Kuu alikubali kusajili tuzo ya malipo ya DOWANS na kuiamuru TANESCO kulipa
fedha hizo pamoja na gharama za uendeshaji kesi.

Wakili wa DOWANS, Bw. Kenedy Fungamtama, alidai kuwa hadi kufikia Novemba 2012, deni lao lilifikia zaidi ya sh. bilioni 122 kutokana na ongezeko la riba ya asilimia 7.5 ya deni la awali.

No comments:

Post a Comment