04 March 2013

Mbowe apewa ushauri wa bure *Viongozi wa dini wamtaka asitishe maandamano



Na Mwandishi Wetu, Mbeya

KAMATI ya Maadili na Haki za Binadamu kwa Jamii inayoongozwa na Maaskofu, Mapadre, Wainjilisti na walimu, imekiomba Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kusitisha maandamano waliyopanga kuyafanya jijini Mbeya wiki hii.

Lengo la maandamano hayo ni kushinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa na Naibu Waziri
Bw. Philipo Mulugo, kujiuzulu katika nafasi zao kutokana na matokeo mabaya ya wanafunzi wa kidato cha nne 2012.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mchungaji William Mwamalanga, alisema kamati
yake inamtaka Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Bw. Freeman Mbowe, kusitisha njia nyingine mbadala ya kufikisha kilio cha wananchi kwa Rais Jakaya Kikwete badala ya maandamano.

“Tunamuomba Rais Kikwete aone umuhimu wa kukutana na Bw. Mbowe ili kulijadili suala hili na kufikia muafaka badala ya kufanya maandamano kwani uchunguzi tuliofanya, tumebaini kuna watu ambao wamepanga kufanya mambo ya ajabu,” alisema.

Mchungaji Mwamalanga aliongeza kuwa, zipo dalili za kuwepo watu hatari katika maandamano hayo ndio maana wameamua kuandika barua ya kuomba kusitishwa maandamano hayo
kwa uongozi wa CHADEMA Taifa.

“Kwanini tugombee fito wakati nyumba tunayojenga ni moja, kimsingi kama maandamano haya yatafanyika yatakuwa makubwa sana kwa sababu suala la elimu linamgusa kila mtu hasa Mtanzania wa chini ambaye amemgharamia mtoto wake kwa kuuza ng'ombe, mbuzi, mazao ya biashara na chakula ili asome,” alisema.

Alisema umefika wakati wa Serikali kutafuta njia mbadala ambayo itampatia  kila Mtanzania haki ya kupata elimu bora si bora elimu na kusisitiza kuwa, Serikali haipaswi kufanya kazi kwa shinikizo la maandamano ya wananchi.

Aliongeza kuwa, utamaduni wa baadhi ya watendaji wasiozingatia viapo, umeanza kuota mizizi nchini hivyo jambo hilo linapaswa kudhibitiwa mapema ili kuepusha maandamano, kumwaga damu.

No comments:

Post a Comment