11 March 2013

Mbowe amaliza mgogoro Ktavi

Na Goodluck Hongo

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw.Freeman Mbowe amemaliza mgogoro mkubwa uliokuwa ukifukuta na kutishia mpasuko ndani ya Chama hicho mkoani Katavi, hadi kusababisha Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), Said Arfi kuripotiwa kutupa kadi yake ya uanachama kwenye kikao cha ndani na kutishia kujitoa,


Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na ofisa habari wa chama hicho Bw.Tumaini Makene alisema mgogoro huo umezikwa rasmi baada ya Mwenyekiti huyo Taifa kulazimika kuingilia kati na kufanya usuluhishi.

 Alisema Desemba mwaka jana kuliripotiwa habari   juu ya kuwepo kwa mgogoro huo, ambapo habari zilidai kuwa katika kikao cha Baraza la Mashauriano la Mikoa ya Rukwa na Katavi (zamani Rukwa) kilichofanyika Namanyere, Nkasi, Arfi ambaye pia ni Mbunge wa Mpanda Mjini, alitupa kadi yake mezani huku akitishia kuvua nafasi zake zote na kujitoa CHADEMA.

Bw.Mbowe alitumia siku nzima katika kusuluhisha pande mbili hizo zilizokuwa zikihasimiana vikali ambapo kundi moja likihusisha uongozi wa chama mkoani humo dhidi ya kundi jingine la baadhi ya viongozi wa BAVICHA wa mkoani humo.

Taarifa zaidi kutoka katika kikao hicho zilidai kuwa Arfi alifikia hatua hiyo baada ya kukerwa na kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Vijana Mkoa wa Rukwa, Laurent Mangweshi kuwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Mbunge huyo alipokea rushwa kutoka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ili CHADEMA kisiweke mgombea katika jimbo la Pinda, Mpanda Mashariki.

Bwa.Mbowe alitumia staili kama alivyomaliza mgogoro wa Karatu na  wale waliokuwa wanahasimiana watajieleza mbele ya mkutano wa hadhara mjini Mpanda ambapo aliwaonya vikali juu ya kuendekeza tofauti binafsi baina ya watu na kuzifanya kuwa ni mgogoro ndani ya chama hicho na kutolea mifano ya maeneo Tarime na Karatu.


Katika kumaliza mgogoro huo Bw.Mbowe alilazimika  kuzionesha pande zote mbili zilivyo na makosa ambapo kwa Upande wa vijana kwa makosa yao ya utovu wa nidhamu kwa viongozi wa chama na ukosefu wa maadili kwa viongozi na wakubwa wao lakini pia viongozi wa chama nao pia wakaoneshwa makosa yao, ikiwemo kuitisha na kukaa kikao batili kisichokuwa na mamlaka ya maamuzi ya nidhamu kisha kuwahukumu vijana wale, bila hata kufuata taratibu, kilisema chanzo chetu kingine.


"ujio wangu si wa kufarakanisha watu bali kuwafanya wapatane, waangalie malengo makubwa zaidi ya chama badala ya ubinafsi na  kufukuzana si dawa, lakini itakapobidi kuwa hakuna njia nyingine, kusingekuwa na msalie mtume kumwondoa mtu bila kujali nafasi yake, kabila lake, dini yake, wala rangi yake, ili kukiokoa CHADEMA Mpanda, Katavi na nchi nzima ili kisirudi nyuma wala kupoteza njia ya kuwapigania Watanzania."alisema Mbowe

Lakini habari kutoka chanzo kingine cha uhakika kati ya pande zilizokuwa zikihasimiana zilisema kuwa makundi hayo mawili yalisameheana kwa kila mmoja kutakiwa na kikao kusahau yaliyopita ikiwemo kufuta maamuzi ya kikao cha Namanyere,

Katika kumaliza mgogoro huo viongozi wa BAVICHA, akiwemo Mangweshi na Juma walilazimika kuomba msamaha kwa makosa waliyokuwa wakituhumiwa nayo, huku pia ikielezwa Makamu Mwenyekiti Arfi na Mbunge wa Viti Maalum, Ana Mallack wakisema yamekwisha na wote waweke maslahi ya chama chao mbele.Jitihada za gazeti hili kumpata Mbowe kuweza kusikia taarifa kuwa chama hicho mkoani Katavi kilikuwa katika mgogoro mkubwa hadi kumlazimu yeye kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda kusuluhisha hazikuzaa matunda

Mgogoro huo ulikuwa mkubwa kwani ulihusisha viongozi wakuu wa chama hicho ambapo  Makamu Mwenyekiti Bara,Bw. Arfi ambapo juhudi za kumtafuta hazikufanikiwa  kwani simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani


No comments:

Post a Comment