11 March 2013

Balozi Sefue aifagilia NHC

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Sefue Ombeni, amelipongeza Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) kwa kufanyakazi nzuri katika miradi yake ya nyumba nchi nzima na kwamba ikikamilika yote baada ya  miaka mitano itasaidia kuboresha maisha ya Watanzania.


Balozi Ombeni alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana alipotembelea NHC kwa lengo la kujionea miradi inayotekelezwa na shirika hilo.  "Hapa Tanzania tuna tatizo la nyumba licha ya kuwa ni hitaji muhimu kwa mwanadamu, lakini tunawapongeza kwa  kazi nzuri inayofanywa na NHC...wanafaanyakazi  nzuri sana," alisema.

Alisema miradi inayotekelezwa na NHC ikikamilika itabadili sura ya miji. "NHC wapo katika njia sahihi kazi yetu (Serikali) ni kuona namna ya kuwaunga mkono ili miradi yao ifanikiwe kwa haraka sana," alisisitiza Balozi Ombeni.

Alipoulizwa kuhusiana na baadhi ya taasisi za Serikali kuwa wadaiwa sugu wa kodi na NHC, Balozi Ombeni alisema watahakikisha fedha zinazotolewa kwenye taasisi za Serikali kwenye bajeti kwa ajili ya kulipa kodi zinatumika kwa ajili hiyo na si vinginevyo.

Alikiri kuwa baadhi ya taasisi zinadaiwa, lakini nyingine zimepunguza madeni tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma.. Awali uongozi wa NHC ulimweleza Balozi Ombeni miradi mbalilmbali inayotekelezwa nchi nzima.

Baadhi ya miradi hiyo imekamilika, inaendelea na nyingine ipo kwenye mipango kwa ajili ya utekelezaji ikiwemo ya vitega uchumi vya shirika, nyumba za kuuza kwa ajili ya watu wenye kipato cha juu kati na cha chini.



No comments:

Post a Comment