20 March 2013

Hukumu wafuasi a ponda

Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kesho inatarajia kutoa hukumu ya washtakiwa wa kesi ya kufanya maandamano haramu kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), inayowakabili wafuasi 53 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Ponda Issa Ponda.

Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa na Hakimu Sundi Fimbo, anayesikiliza ambapo upande wa mashtaka ulikuwa ukiwakilishwa na wakili wa Serikali, Bernad Kongola, wakati upande wa utetezi unawakilishwa na wakili Mohamed Tibanyendela.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi saba na vielelezo mbalimbali ambapo upande wa utetezi, washtakiwa hao walijitetea wenyewe.

Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya maandamano haramu Februari 15 mwaka huu kwenda kwa DPP, licha ya Jeshi la Polisi kukataza kufanyika kwa maandamano hayo.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao wanadaiwa kufanya maandamano haramu kwenda katika Ofisi ya DPP ili kumshinikiza atoe dhamana kwa Shekhe Ponda na mwenzake Shekhe Mukadamu Swalehe.

Katika maelezo ya awali, washtakiwa hao walidaiwa kuwa awali polisi walitoa zuio la maandamano hayo lakini walikaidi ambapo siku ya tukio, polisi waliwaamuru kutawanyika katika mikusanyiko waliyokuwa wakiifanya na kukaidi ndipo wakakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Katika maelezo hayo, mshtakiwa wa kwanza Bw. Salum Makame, alikiri kukutwa na kisu na kipaza sauti lakini akakana kuwa hakuwa mfuasi wa Shekhe Ponda.

No comments:

Post a Comment