11 February 2013

Watumishi 4 wasimamishwa kazi, madiwani wamshukia DED


Na Ramadhan Libenanga, Mvomero

BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, limewasimamisha kazi watumishi wanne wa halmashauri hiyo pamoja na kupiga kura ya kutokuwa na imani
ya kufanya kazi na Mkurugenzi wa halmashauri (DED),
kutokana na tuhuma ya ubadhirifu wa sh. milioni 58.


Azimio hilo limefikiwa na madiwani hao katika kikao maalumu baada ya kupokea taarifa ya ukaguzi wa fedha za miradi ya
maendeleo wilayani humo.

Akizungumza katika kikao hicho mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Bw. Jonas Vanzeland, alishangazwa kuona miradi mingi ya maendeleo haijatekelezwa wilayani humo wakati tayali ilitengewa fedha zake.

“Kwa mfano, miradi ya kilimo na ujenzi utekelezwaji wake umekuwa wa kusuasua kumbe wanakula pesa za Serikali,”
alisema Bw. Vanzeland.

Aliongeza kuwa, Kamati ya Fedha ya madiwani ilimuagiza Mkaguzi wa Ndani kufanya ukaguzi na kubaini matumizi mabaya ya fedha za halmashauri yasiyoendana na kanuni, sheria, taratibu za utoaji fedha.

Alisema ukaguzi wa ndani umebaini kuwa, katika akaunti ya maendeleo zaidi ya sh. milioni 469.7 zimetumika bila kuonesha matumizi yake jambo ambalo ni kinyume na sheria ya matumizi
ya pesa za Serikali.

Bw. Vanzeland alisema, kasoro nyingine iliyojionesha ni matumizi ya zaidi ya sh. milioni 8.8 kuanzia Septemba 10 hadi Novemba 11,2012 bila maelezo yoyote.

“Baraza la madiwani kwa pamoja limedhamilia kukomesha vitendo vya ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo katika halmashauri kwa watendaji...ukaguzi huu umehusisha miezi michache,” alisema.

Aliongeza kuwa, lengo ni kufanya ukaguzi wa matumizi ya fedha
za miradi kuanzia 2009 hadi 2013 na watakaobainika hata kama watakuwa wameamishwa, watarudishwa kujibu tuhuma.

Waliosimamishwa ni Bi. Estar Majagi (Ofisa Mipango), Bw. John Kuyi (Mhasibu Matumizi), Bi. Anastazia Shosho na Bw. Stevin Tibenda (Watunza Fedha).

Wakati huo huo, Bw. Vanzeland na baraza hilo, wamedai kutokuwa na imani na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bi. Sala Linuma na kudai pengine anahusika moja kwa moja na ubadhirifu huo.

“Niko tayari kuachia Uenyekiti wa halmashauri hii, kama tutaendelea kufanya kazi na Mkurugenzi anayelea ubadhirifu,
kwa mujibu wa sheria Baraza la Madiwani halina vifungu vya kumfukuza Mkurugenzi lakini tumeandika barua kwa Mkuu
wa Mkoa, nakala tumepeleka kwa Waziri husika,” alisema.

No comments:

Post a Comment