06 February 2013

Jela miaka 2 kwa kuua akidai sh. 4,000



Na Pendo Mtibuche, Dodoma

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma, juzi ilimuhumuku mkazi
wa Dodoma Mjini, Yohana Chipini (23), kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Alord Ndeshio, bila kukusudia wakati akidai sh. 4,000.


Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Mary Shangali baada ya mshtakiwa kukiri kosa na kumtia hatiani.

Jaji Shangali alidai kuwa, amezingatia maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka pamoja na utetezi kuhusu chanzo cha mauaji hayo ambacho ni ugomvi uliotokea kati yao wakati mshtakiwa alipokwenda kumdai marehemu fedha zake.

Aliongeza kuwa, baada ya ugomvi huo mshtakiwa aliokota kipande cha ubao au kitu kinachoaminika kuwa kipande cha chuma na kumpiga nacho marehemu kichwani.

“Adhabu ya kuua bila kukusudia ni kifungo cha maisha lakini kutokana na mazingira yalivyoonyesha na utetezi wa mshtakiwa, Mahakama imempunguzia adhabu na hivyo atatumikia kifungo
cha miaka miwili gerezani,” alisema.

Kabla ya hukumu hiyo, wakili wa mshtakiwa, Steven Kuwayawaya, aliiomba mahakama impunguzie adhabu mshtakiwa akidai kosa hilo ni la kwanza na amekiri kosa.

Awali, ilidaiwa na upande wa mashtaka kuw,  mshtakiwa alitenda kosa hilo mwaka 2012 katika barabara ya Bahi, Manispaa ya Dodoma.

No comments:

Post a Comment