28 February 2013

Wakulima wafuate ushauri wa wataalamu- TMA



Na Goodluck Hongo

MAMLAKA ya hali ya hewa nchini (TMA)imewataka watumiaji wa taarifa za hali ya hewa nchini wakiwemo wakulima kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika kotokana na kuwepo kwa mvua za wastani katika miezi mitatu ijayo.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam  jana mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo Dkt.Agnes Kijazi alisema kutokana na kuwepo kwa mvua za wastani katika miezi mitatu ijayo ni vizuri watumiaji wote wa taarifa hizo wakafuata ushauri kutoka katika sekta hizo.

Alisema mwelekeo wa msimu wa mvua za Machi hadi Mei,mwaka huu unaonesha kuwa maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka yaani Ukanda wa ziwa Victoria,Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na Pwani ya Kaskazini yanatarajiwa kupata mvua za wastani.

Alisema mvua zinazoendelea kunyesha kwenye maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka yaani maeneo ya Magharibi, nyanda za juu kusini magharibi zinatarajiwa kuwa ni za chini ya wastani katika maeneo mengi isipokuwa katika Mikoa ya Njombe,Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa Mikoa ya Mbeya, Iringa na Morogoro ambayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani.

"Tungependa kuwaambia kuwa katika utabiri huu wa miezi mitatu ijayo tunatumia sana kuwepo kwa joto la bahari ambapo viashiria vikubwa ni kuwepo kwa joto la bahari la wastani katika maeneo ya mashariki mwa bahari ya Atlantic na joto la wastani magharibi mwa bahari ya Hindi huku upepo wenye unyevunyevu hafifu kutoka misitu ya Congo kuvuma kuelekea nchini,"alisema Dkt.Kijazi.

Alisema mwelekeo wa mvua za mwezi Machi hadi Mei mwaka huu katika  kanda ya ziwa katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu mvua zitaanza kunyesha kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi Machi na baadhi ya mikoa hiyo mvua zitaanza wiki ya pili ya mwezi machi ambapo itapata mvua za wastani.

Dkt.Kijazi alizitaka taasisi za maafa na wadau husika na hilo kuchukua hatua muafaka za maandalizi ya kukabiliana na majanga ya hali ya hewa yanayoweza kutokea ambapo katika miezi mitatu ijayo mvua zitakuwa ni za wastani katika maeneo mengi ya nchi.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa utabiri wa hali ya hewa nchini Dkt.Hamza Kabelwa alisema wao wamegawanya mikoa katika kanda mbalimbali na utabiri unaotolewa si kwamba lazima mvua inyeshe siku chache zijazo bali utabiri wao unalenga ndani ya miezi mitatu kutokea kwa  kitu hicho

Alisema utabiri ambao mamlaka hiyo uliutabiri wa mwaka 2012 kwa miezi ya Oktoba hadi Desemba ulikuwa ni sahihi zaidi kwani ilitokea kama walivyotabiri ambapo na mwaka huu wa 2013 nao wanatarajiwa kwa miezi mitatu ijayo ya Machi na Mei 2013 hali itakuwa hivyo kwani kitu kikubwa ambacho wanatumia ni joto la bahari.

No comments:

Post a Comment