28 February 2013

Avua nguo asikamatwe na Dawasco


Na Heri Shaaban

OPERESHENI ya kuwasaka wezi wa maji Dar es Salaam, juzi imechukua sura mpya baada ya mkazi wa Tandale Chama, wilayani Kinondoni ambaye ni mwanamke (jina tunalo), kuvua nguo zote.

Chanzo cha mwanamke huyo kuvua nguo ni baada ya kuuona msafara wa Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Meck Sadiki na Maofisa
wa Shirika la Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO), ambao walimkuta akiuza maji aliyojiunganishia kiholela.

Hata hivyo, Ofisa wa DAWASCO ambaye ni mwanamke alilazimika kumkamata na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi waliokuwa katika operesheni hiyo.

Operesheni hiyo ilifanyika kwenye eneo la Kagera, Tandale Chama, Mkwajuni na Bonde la Mkwajuni ambapo vifaa mbalimbali ambavyo vilikuwa vikitumika kuunganisha maji vilikamatwa.

Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Sadiki alisema operesheni hiyo imefichua mambo mengi yanayofanywa na wananchi aliowaita wahujumu uchumi kwa kujiunganishia maji kiholela bila kuyalipia.

Alisema asilimia 36 ya maji yamekuwa yakipotea kutokana na baadhi ya watu kujiunganishia kichume cha sheria.

“Leo kwa macho yangu nimeshudia wezi wawili katika oparesheni hii, nakuomba Mkuu wa Wilaya hii (Jordan Rugimbana), kesho mchana (leo), unikabidhi majina ya wezi wa DAWASCO .

“Wizi huu hauna tofauti na wauzaji dawa za kulevya hivyo
tuchukue hatua mapema kudhibiti hali hii,” alisema Bw. Sadiki na kuongeza kuwa, maji yanayopotea ni sawa na lita milioni 100.

Aliwagiza DAWASCO wajitazame upya kwa watendaji wake ambao wanalihujumu shirika hilo na kuweka mikakati ya kudhibiti tatizo hilo kwa kuunda chombo cha maadili ili watendaji wabovu wawajibishe.

1 comment:

  1. Hakika, operation hii inatakiwa kuwa endelevu, sababu nchi hii kila mtu anajiamulia tu kuwa fisadi kwa size yake. Hii inasababisha kurudisha nyuma maendeleo, na kutesana wenyewe.

    ReplyDelete