27 February 2013

Wahusika mauaji ya vikongwe, albino wasifumbiwe macho


Na Bryceson Mathias

KWA muda mrefu sasa nchi yetu imekuwa ikikabiliwa na wimbi la mauaji ya ndugu zetu vikongwe na walemavu wa ngozi albino.

Pamoja na kulaaniwa na wanajamii wengi na hatua mbalimbali ambazo serikali imejaribu kuzichukua, wimbi la mauaji limezidi kuenea na hivi leo,wenzetu hawa hawana amani tena ndani ya nchi, maana.Maisha yao yanatishiwa kila kukicha.

Wimbi hili limezidi kuipaka nchi yetu matope kama wana jamii, hivyo,hatuwezi kukaa kimya ni wazi kwamba juhudi za ziada zinahitajika kutoka serikalini ili kukomesha mauaji hayo ambayo msingi wake ni imani potofu kwamba viungo au sehemu mbalimbali za mwili wa vikongwe au albino ni njia mojawapo ya kujipatia utajiri

Utajiri kwa tafsiri rahisi ni hali ya mtu kuwa na mali nyingi na ambazo humwezesha kuishi kwa namna anavyotaka yeye.

Kwa mfano wakati fulani Watanzania walishuhudia ujio wa mmiliki wa timu ya Chelsea aliyekodi hoteli nzima pale mjini Arusha na kwamba ndege aliyokuja nayo ilitosha zaidi ya abiria mia kadhaa. Pengine kwa tafsiri rahisi,huyo ndiye anaweza kuitwa tajiri.

Lakini kwa upande wangu nahoji, ukweli ni upi kuhusu utajiri utokane na vikongwe na albino? Kwa kujibu hili inabidi tutazame nini chanzo hasa cha ndugu zangu hawa kuhusishwa na utajiri huo usiokuwepo.

Historia yake fupi imebebwa na waganga wa kienyeji wakiipenyeza dhana hii kwa kupitia wachache wenye uchu wa madaraka, uongozi na au utajiri. Kwa kuwa waganga hawa wa kienyeji na wao ni watafutaji wa maisha kama mtu mwingine yoyote yule, kwa kujua au kutokujua walianzisha dhana hii ya kuwa wanao uwezo wa kubadilsha viungo vya albino na kumletea mtu utajiri kwa kupitia kazi yake.

Kwa mfano mtangazaji wa Ajzeera, Yvone Ndege alipomhoji mmoja wa wana jamii mwenzetu kutoka kanda ya ziwa alifafanua akidai kuwa, wanahusika na vioungo hivyo husema, wanapovitumia katika shughuli zao za uvuvi hupata samaki mara dufu.

Tujiulize ni kwa kiasi gani madai hayo yana ukweli, bado ni kitendawili tu!.Ninachokiamini mimi ni kwamba, kwa makosa wanayofanya ya kuua vikongwe na albino bila huruma, hawajui kama wanapunguza nguvu kazi na kurudisha nyuma maendeleo badala ya kwenda mbele kama baadhi yetu wanavyodhani; na licha ya kupata dhambi wanaambulia laana mbele za mwenyezi Mungu.

Kama kweli viungo hivyo vingekuwa vinaleta utajiri basi albino wenyewe kwa upande wao wengekuwa matajiri sana badala ya kuleta hasara ya uvunaji wa viungo vya albino na vikongwe kwa ujumla wao wanavyofanya.

Nimetumia neno uvunaji ili kuleta hasa maana ya kile kinachofanywa na wahuni hawa kwani tendo hilo hufanyika kama vile watu hawa (albino na vikongwe) ni mashamba na mali za kundi hilo chafu linalopaswa si kulaaniwa tu bali likionekana lifae kuangamizwa.

Albino huviziwa hasa nyakati za usiku au hata kuvamiwa nyumbani, wanaomkamata albino au vikongwe, hufanya hivyo pasipo kujali maumivu anayoyapata binadamu huyu, mkono, mguu, kidole, kichwa au sehemu nyingine wanapokatwa hata kama ni sehemu za siri, huchukuliwa na mhuni huyu na kutoweka na sehemu hizo huku albino akiachwa akivuja damu.

Zoezi hili hufanyika sana vijijini ambako hata huduma za afya  hupatikana mbali kidogo, hivyo kitendo cha kumchukua majeruhi huyu na kumkimbizia zahati au hospitali hakusaidii kitu kwani mauti humkuta njiani au wakati mwingine hapo hapo kwenye eneo la tukio.

Kama wahuni hao hufanya hivyo kwa albino na vikongwe kwa nia kupata utajiri usiokuwepo, swali langu wanaowaua watu kwenye mikutano ya hadhara wana lengo gani? Je wanataka wawe wanasiasa bora? Je wanataka waendelee kutawala? Je  ni sadaka inayotolewa mahali fulani walikoahidiwa kufanywa hivyo ili waishi?

Kila mara najiuliza na ninaumia sana, hatua hizo zina makusudi gani kwa jamii? Nataka kujua damu ya watu hawa inapelekwa wapi? Yu mkini kuna wenzetu wanadhani wanafaidika na umwagaji wa damu hizi, lakini masikitiko yangu isije ikawa nao wamedanganywa kama walivyodanganywa wengine kwamba, wakiwaua vikongwe na albino, viungo vyao vinawapa utajiri.

Aidha naomba na wewe ujiulize je mauaji yanayofanywa kwenye mikutano inaendeleza kupata vyeo kwa wauaji? Je yanaendeleza watu waendelea kuwa kwenye nafasi walizonazo? Je wanataka waendelee kuwa watoto wasife? Je wanataka wawe vijana wasizeeke? Je wanataka waendelee kuwa wawekezaji wa nyadhifa walizonazo?.au wanaowatuma ndio wanaofaidika?.

Tafakali na uchukue hatua, ili uwe mmoja wa wanaojiuliza maswali na ikibidi ufanye maamuzi ni nini kifanyike ili kukomesha hali hii na kupata majibu tata ya mauaji ya kwenye mikutano ambayo sasa inarithi ya vikongwe na albino ambapo watekelezaji husema wanataka utajiri. Je mauaji ya raia mikutanoni lengo lake ni nini? Lakini naonya wale mnaotumia mtindo huo wa uuaji tumewatambua, mnaonekana na kama si na sisi lakini yuko muumba anayewaona; acheni mtindo huo umepitwa na wakati, na msipoacha zamu yenu inafuata mbele za Mungu.

nyeregete@yahoo.co.uk
0715-933308No comments:

Post a Comment