26 February 2013

Waandishi, Wahariri lipo la kujifunza kwa hofu ya kutekwa



SAKATA la wananchi mkoani Mtwara kupinga ujenzi wa bomba
la gesi kutoka Kijiji cha Msimbati, mkoani humo hadi jijini Dar es Salaam, huenda likaifikisha nchi mahali pabaya.

Hali hiyo inatokana na msimamo wa wananchi kupinga ujenzi huo wakidai kuwa, gesi iliyopatikana mkoani humo ni rasilimali pekee inayoweza kubadilisha maisha yao hivyo hawapo tayari kuona ikisafirishwa ili kunufaisha wananchi wa mikoa mingine.

Februari 21 hadi 22 mwaka huu, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), uliandaa kongamano la nane la Wahariri na Waandishi wa habari ambalo hufanyika kila mwaka katika mikoa tofauti.

Kongamano hilo ambalo huzungumzia suala zima la huduma za afya, mwaka huu lilifanyika mkoani humo ambapo Wahariri na waandishi, walilazimika kuondoka alfajiri kutokana na hofu ya
kutekwa na watu wanaopinga gesi hiyo isisafirishwe.

Zipo taarifa zinazosema dhamira ya wana Mtwara walitaka kuzungumza na waandishi pamoja na Wahariri ukweli juu
mgogoro unaohusiana na gesi kati yao na Serikali.

Taarifa nyingine zinasema kuwa, kilio cha wananchi hao kwa waandishi na Wahariri wa vyombo vya habari ni juu ya habari wanazoandika kuhusu suala hilo ambazo zimelenga kupotosha
umma kuwa sakata hilo limekwisha wakati bado linaendeleea.

Sisi tunasema kuwa, hofu iliyojitokeza kwa wanahabari ambao walilazimika kuondoka alfajiri ni changamoto ambayo itawafanya warudi Mtwara kufuatilia sakata hilo kwa kina ili kile ambacho watakiandika, kiwe na tija kwa wananchi na Serikali pia.

Suala la gesi mkoani humo ni hoja nzito ambayo utatuzi wake, utatokana na busara za Serikali pamoja na vyombo vya habari kufanya kazi zao bila kuhusisha ushabiki wa kisiasa.

Hivi sasa, wakazi wa Mtwara ni wasomi wazuri wa magazeti, kuangalia na kusikiliza habari zinazorushwa katika redi na televisheni hivyo kama vyombo vya chombo cha habari
vitaandika habari za gesi kiushabiki, upo uwezekano wa
kutokea vurugu zinazoweza kuhatarisha usalama wa nchi.

Imani yetu ni kwamba, Serikali ambayo sisi tunaamini ni sikuvu, itawasikiliza wakazi wa Mtwara ili ndoto yao ya kuwa na maisha
bora iweze kutimia kupitia rasilimali ya gesi ambayo wao wanaamini ndio inayoweza kuufanya Mkoa huo kuwa wa
kisasa kama ilivyo mikoa mingine.

Baadhi ya mikoa yenye rasilimali kama madini pamoja na vivutio vya utalii, hivi sasa imepiga hatua kubwa ya maendeleo hivyo umefika wakati wa wana Mtwara kutimiza ndoto yao.

Umefika wakati wa Serikali kuandaa utaratibu wa kufanya mikutano na wananchi ili kusikiliza kilio chao na kuwapa majibu ambayo kwa namna moja au nyingine, yanaweza kusaidia wakabadili msimamo wao tofauti na ilivyo sasa.

No comments:

Post a Comment