26 February 2013

Mikakati thabiti inahitajika kumaliza tatizo la utapiamloNa Rachel Balama

TANZANIA ni kati ya nchi ambazo inakabiliwa na changamoto kubwa ya ugonjwa wa utapiamlo.

Serikali kwa kushirikiana na sekta mbalimbali za huduma ya afya zimekuwa zikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa ugonjwa huo unapungua hapa anchini.

Kutokana na jitihada hizo zimeweza kufanikiwa na kupunguza idadi kubwa ya watoto wanaokufa kwa ugonjwa huo hapa nchini kwa kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka nchini na nchi za nje.

Katika muongo wa miaka 10 uliopita, zaidi ya watoto 600,000 wenye umri chini ya miaka 5 wanakisiwa kufa kwa kukosa lishe ya kutosha.

Ingawa utapiamlo husababisha vifo, ni kwa nadra sana vifo hivyo husababishwa na kushinda na njaa.

Watoto wanakufa kwa sababu milo yao haina virutubisho vya msingi vinavyohitajika kujenga mfumo imara wa kinga za mwili na kuwaweka wenye afya.

Pindi mtoto mwenye utapiamlo anapougua uharisha, malaria au homa ya mapafu anakuwa na uwezekano mkubwa wa kufariki.

Vifo vyao vingeweza kuepukika iwapo watoto hawa wangelishwa vyakula vyenye ubora wa kutosha lakini utapiamlo umebaki ukipuuzwa huku ukiendelea kuongeza kasi ya kuteketeza watu.

Utapiamlo unadhoofisha uchumi.Wakulima na wafanyakazi wengine, hasa wanawake,wanadhoo fika na kudumaa, kutokana na kukosa vyakula viletavyo nguvu mwilini pamoja na maradhi ya upungufu wa damu.

Kutokana na utapiamlo, wakulima hushindwa kutumia nguvu nyingi hivyo kupelekea mavuno kidogo na kupungua kwa tija ya wafanyakazi.

Utapiamlo pia unachangia upotevu wa fursa za kiuchumi, kwani watu wazima wenye ukuaji uliodumaa wa ubongo kutokana na kukosa virutubisho kipindi cha utoto wana uwezo mdogo wa kubuni na kuchangamkia fursa mpya za maendeleo.

Asilimia 42 ya ulemavu kwa watoto nchini umesababishwa na magonjwa yatokanayo na ukosefu wa lishe bora katika miaka miwili tangu kuzaliwa kwake.

Mkoa  wa Lindi ni miongoni mwa mikoa 30 ya Tanzania ambapo una jumla ya watu 596,760, na inakadiriwa asilimia 51 ya watu wake wako katika kiwango cha chini cha umaskini cha Taifa.

Mkoa huo una viashiria vya hali ya lishe bado vipo chini kutokana na takwimu za TDHS, pamoja na kuonyesha kuwa vifo vya watoto wadogo vimepungua kutoka asilimia 50 mpaka asilimia 30 kwa mwaka 2010 ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Mratibu wa Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Lindi,Nancy Mwailupe,anaeleza kuwa taarifa za TDHS inaonyesha kuwa watoto wanaoishi vijijini ni rahisi kuwa na udumavu kwa asilimia 45 kuliko wale wanaoishi mijini kwa asilimia 32, wakati asilimia 64.8 ni wakondefu na aslimia 21 wana uzito pungufu.

Pia kwa hali ya lishe mkoa wa Lindi ni mkoa wa pili kwa watoto wenye udumavu kwa asilimia 54, ukiongozwa na mkoa wa Dodoma wenye watoto asilimia 56 wenye udumavu.

Anasema mkoa huo pia una watoto wa umri wa miezi 0-59 ambao wana uzito pungufu kwa asilimia 23.7, watoto wa umri wa miezi 0-59 wana Anemia ambao sawa na asilimia 76.8,

Anasema wanawake kati ya umri wa miaka kati ya 15-49 wana Anemia sawa na asilimia 46.3 na kaya zenye watoto wa umri wa miezi 6-59 ambao wanatumia chumvi yenye madini joto ni asilimia 8.9.

Hali ya kiuchumi kwa mkoa huo inategemea sana kilimo na uvuvi, ambapo asilimia 87 ya wakazi wanategemea kilimo cha mvua.

Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa mikoa yenye fursa nzuri ya kilimo, uku wilaya ya Ruangwa wakitumia ardhi kwa kilimo kwa asilimia 34 tu, uku wakiwa na eneo la hekta 4332 la kilimo cha umwagiliaji ambapo kati ya hizo hekta 80 tu ambayo sawa na asilimia 1.8 ambazo kwa sasa ndo zinatumika kwa kilimo cha umwagiliaji.

Pamoja na mkoa huo kutegemea kilimo kama shughuli kuu za kiuchumi,wanawake wanaonekana kuwa wazalishaji wakubwa lakini wanaume wanaonekana kuwa wasimamizi na wamiliki wa mazao hayo baada ya mavuno, matatizo ya kijinsia (kama talaka) ni tatizo kubwa linalojitokeza kipindi cha mavuno ambapo wanaume wengi wanaoa wake wengine baada ya kuona wana mazao mengi.

Hali hiyo huchangia kaya nyingi zinazoongozwa na wanawake kukosa chakula cha kutosha cha kulisha kaya zao kutokana na chakula kingi kuchuliwa na wanaume. Kwa mkoa huu kaya masikini zenye watoto wa umri wa miezi 6-24 wanapata tatizo la kulakula mlo wa aina moja katika kipindi cha kilimo.

Hali halisi inaonesha kuwa, ukosefu wa virutubisho (kama madini) na kutonyonyesha maziwa ya mama kwa miezi sita mfululizo ni tatizo sugu linalochangia kuwepo kwa utapiamlo mkali kwa watoto wadogo.

Kwa kutambua umuhimu wa lishe katika kupunguza tatizo la utapiamlo nchini Shirika la Kimataifa la Save The Children limezindua mradi ujulikanao kama 'Harnessing Agriculture for Nutrition Outcomes (HANO)' kwa ajili ya Kilimo na Lishe.

Kwa upande Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi,Dkt.Nassoro Hamidi, akizundua mradi wa HANO,anasema mradi huu unalenga kuboresha lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Anasema lishe bora ni jambo muhimu kwa Taifa,  juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali, Mashirika ya Kimataifa, Asasi za Kiraia na Wadau wa Maendeleo ni kuboresha hali ya Lishe Kitaifa ili kupambana na utapiamlo.

Anaeleza takwimu zinaonyesha hali ya utapiamlo kitaifa ni asilimia 42, Mkoa wa Dodoma ni wa kwanza kwa hali mbaya ya utapiamlo kitaifa kwa asimilia 56 ukifuatiwa na Mkoa wa  Lindi wenye asilimia 54 ya watoto wenye utapiamlo (udumavu) chini ya umri wa miaka mitano.

Anasema takwimu hizi ni kubwa kuliko hata wastani wa  kitaifa ambao ni asilimia 42 ya watoto wenye tatizo la utapiamlo (udumavu).

Madhara ya tatizo la utapiamlo ni makubwa sana katika ukuaji wa mtoto kimwili na kiakili na hii inapelekea kuandaa taifa la kesho ambalo halitakuwa na uwezo mzuri katika kufikiri, kupanga na kutekeleza mipango na mikakati mizuri kwa Maendeleo ya Taifa.

Ili kuwa na maendeleo thabiti katika juhudi hizi na kupunguza vifo vya akina mama na watoto vinavyosababishwa na utapiamlo, sera inahimiza ushirikiano wa sekta zote kuhakikisha kunakuwepo na uhakika wa chakula na lishe kwa jamii zetu.

Serikali ya Tanzania imepata mafanikio mazuri hasa kwenye kuweka misingi ya kupambana na janga la utapiamlo.

Anasema inahitajika bajeti ya kutosha kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya ili kuweza kutekeleza mipango hii mizuri ambayo italeta manufaa kwa watoto wetu pamoja na jamii nzima kwa ujumla.

Save the Children ni miongoni mwa wadau wanaoshirikiana na Serikali yetu kuboresha lishe na afya hususani kwa akina mama walio katika umri wa kuzaa pamoja na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Anasema katika Mkoa wa Lindi wamekuwa wakishirikiana na Halmashauri za Wilaya ya Ruangwa, Halmashauri ya Lindi na Kilwa kuboresha afya ya mama na mtoto chini ya miaka mitano kwa kipindi cha miaka minne sasa.

Anasema kwa kipindi hiki wameweza kuongeza wigo wa Miradi yao na kuweza kupunguza utapiamlo kwa kina mama na watoto suala ambalo bado halina wadau wengi katika mkoa huo.

Mradi wa HANO ambao unalenga kuboresha lishe kwa akina mama wenye umri wa kuzaa na watoto wenye umri chini ya miaka mitano utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika Wilaya ya Rungwa na Halmashauri ya Lindi.

Anasema mradi huo utakuwa ni chachu muhimu katika kuhamasisha jamii husika kuweza kujishughulisha zaidi katika kilimo cha mazao mbalimbali kwa uhakika wa lishe bora katika ngazi ya kaya.

Anasema ni mradi ambao utekelezaji wake utashirikisha idara mbalimbali za halmashauri husika pamoja na asasi za kijamii ili kuweza kufikia jamii husika kwa nguvu ya pamoja ambayo itakuwa endelevu hata baada ya muda wa mradi kuisha.

Anasema elimu juu ya masuala ya kilimo bora, uhifadhi salama wa mazao, jinsi ya kuandaa chakula na kulisha watoto kuanzia anapozaliwa mpaka anapofikisha umri wa miaka miwili ni maeneo muhimu yatakoyowekewa mkazo ili kupunguza tatizo la udumavu ambalo halirekebishiki tena baada ya umri wa miaka miwili.

Anazitaka idara zote zitatoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza Mradi huu na pia itakuwa ni fursa ya halmashauri husika kuanza kuingiza shughuli zinazoboresha lishe hususani kwa kina mama na watoto katika mipango yao ya kila mwaka ili kufanya machakato huu uwe endelevu na wa manufaa kwa jamii zetu.

Mkurugenzi wa Miradi wa Save the Children, John Kalage, anasema katika utekelezaji wa mradi huo kwa kipindi cha miakamitatu utagharimu zaidi ya sh.bilioni mbili.

Kalage anataja malengo ya mradi huo kuwa ni kuimarisha, kuongeza kiwango cha lishe bora kwa akina mama na watotio waliochini ya umri wa miakamitano, kukuza uwezo wa halmashauri kupanga na kutekeleza miradi inayoweza kuboresha lishe.

Pia kusaidia utafiti na namna bora ya kilimo na lishe ambapo utafiti utafanyika ili kuona namna gani kilimo na lishe kitauganishwa ili kuboresha lishe.

Anataja baadhi ya faida ambazo zitapatikana kupitia mradi huo kuwa ni kuongezeka kwa akina mama wanaonyonyosha watoto kwa muda unaotakiwa wa miezi sita bila kumpa kitu chochote.

Pia kuongezeka kwa akina mama ambao watawapa watoto wao chakula cha ziada baada ya muda wa miezi sita ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee.

Ulaji wa vyakula vyenye virutubisho vitaongezeka katika ngazi ya kayapamoja na kuongezeka kwa kiwangocha akina mama na baba ambao watazalisha chakula na kuhifadhi vizuri kwa asilimia 50.

Anasema mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa mipango ya wilaya katika utekelezaji wa masuala ya lishe na mashirika yatakuwa na uwezo wa kutangaza masuala ya lishe.

Kalage,anasema kuwa elimu juu ya masuala ya kilimo bora,uhifadhi salama wa mazao,jinsi ya kuandaa chakula na kulisha watoto kuanzia anapozaliwa hadi anapofikisha miaka miwilini maeneo yatakayowekewa mkazo lengo ikiwa ni kupunguza tatizo la kudumaa kwa watoto kutokana na lishe duni, tatizo ambalo halirekebishiki baada ya mtoto kuvuka umri wa miaka miwili.

Anasema suala lishe bora linawahususu watu wote bila kujali kipato chake  hivyo ili kutokomeza tatizo hilo elimu zaidi lazima itolewe .

No comments:

Post a Comment